1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bado njia ni ndefu

6 Februari 2007

Kuanzisha tena utaratibu wa kutafuta amani Mashariki ya Kati – ziara ya Kansela Merkel katika nchi mbali mbali za eneo hili. Alipotembelea Abu Dhabi, Bi Merkel alitoa hotuba juu ya sera za Umoja wa Ulaya kuelekea Mashariki ya Kati na kusisitiza kuwa inabidi kufikiria mustakabali wa muda mrefu. Yafuatayo ni maoni ya mwandishi wetu wa mambo ya Mashariki ya Kati, Peter Philipp.

https://p.dw.com/p/CHKh

Wengi wameshindwa kuutatua mzozo wa Mashariki ya Kati, kwa mfano rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton. Kwa hiyo, Angela Merkel, bila shaka, hakuwa na matumaini makubwa kushinda pale ambapo wengine wameshindwa. Lakini ziara yake ndefu zaidi tangu kuingia madarakani ni hiyo ya kwenda eneo la Mashariki ya Kati. Ujumbe wake ni wazi: Anataka utaratibu wa kutafuta amani uanzishwe tena na Ujerumani na Umoja wa Ulaya ziko tayari kuchangia iwezekanavyo ili lengo hilo lifikiwe.

Hadi hapa hatua hiyo si mbaya, kwani tangu chama cha Kiislamu cha Hamas kushinda katika uchaguzi, Ulaya haijachukua hatua ya maana ya kujitahidi mzozo huu utatuliwe. Na kwa upande wa Marekani, baada ya Bill Clinton aliyejaribu mara nyingi kupatanisha, mrithi wake, George W. Bush, hajajiingiza sana, au iwapo, basi aliiunga mkono Israel.

Vita vya Irak, mzozo wa mradi wa kinyuklia wa Iran, ghasia nchini Lebanon na mapigano kati ya vyama vya Fatah na Hamas – haya yote yalizidisha ukali wa mivutano. Lakini wakati huo huo yalisababisha taa za tahadhari ziwashwe – maana yake: sasa inabidi hatua zichukuliwe haraka. Kutokana na kuuunga mkono upande mmoja, Marekani haifai kuanzisha upya utaratibu wa kutafuta amani. Ulaya lakini ina fursa nzuri zaidi, hata ikiwa ni wazi kwamba bila ya Marekani haitafaulu. Na kwanza kabisa inategemea nia ya pande husika zenyewe.

Kimsingi basi ni kusifiwa Angela Merkel kwa vile anajitolea kuzileta pamoja tena pande nne zinazoshughulikia amani ya Mashariki ya Kati, yaani Umoja wa Ulaya, Marekani, Urusi na Umoja wa Mataifa. Lakini mkutano wao wa kwanza baada ya miezi mingi ulionyesha kuwa kwanza lazima Wapalestina wamalize mivutano yao na wakubali lengo la maafikiano na Israel. Hapa Ulaya haiwezi kufanya chochote, bali inaweza kuzisaidia Misri na Saudi-Arabia katika juhudi zao za kupatanisha.

Kwa kuangalia hivyo, ziara ya Kansela Merkel ya kuwatembelea viongozi wa Misri na Saudi-Arabia ulikuwa mchango mzuri, ila ni mdogo. Mchango huu ni kuonyesha tu kuna makubaliano ya kimataifa mzozo huu utatuliwe. Lakini kuanzia hapa hadi utaratibu wa kutafuta amani uanze kuingia mbioni bado ni njia ndefu.

Na juu ya hayo: matatizo ya Libanon, mzozo kuhusu mradi wa kinyuklia wa Iran na hali ilivyo nchini Iraq yamewekwa kando kwenye ziara hiyo ya Angela Merkel. Bado basi kuna kazi chungu nzima.