1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Adhabu ya kifo kwa Saddam Hussein, Rais wa zamani wa Iraq itatekelezwa kwa vyovyote vile.

27 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCfo

Msemaji wa rais wa Iraq amesema uamuzi wa mahakama ya rufaa kuhusu kutekelezwa kwa adhabu ya kifo kwa rais wa zamani wa Iraq Saddam Hussein ni wa mwisho wala hauhitaji idhini ya Rais Jalal Talabani.

Tangazo hilo lina maana kwamba jitihada za Saddam Hussein kukwepa adhabu ya kifo zimefikia kikomo.

Maoni mbali mbali yametolewa kuhusu hukumu hiyo.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Italia, Massimo D’ Alema, amesistiza kwamba Umoja wa Ulaya unapinga adhabu ya kifo ilhali Marekani imeusifu uamuzi huo ikiutaja kuwa hatua muhimu ya maendeleo ya Iraq.

Balozi wa Uhispania mjini Baghdad, Ignacio Ruperez, amesema hukumu hiyo haisaidii kitu kwa wakati huu wala siku za usoni za Iraq.

Iganicio Ruperez amesema:

"Hukumu hii mpya, yaani kuthibitishwa kwa adhabu ya kifo, sio tu si nzuri, lakini haina faida. Haileti manufaa yoyote kwa Iraq kumfanya kufa shahidi au shujaa. Nchi yenyewe ina matatizo chungu nzima na hili sasa ni jingine"

Mtawala huyo wa zamani wa Kiimla na washtakiwa wengine wawili walihukumiwa adhabu ya kifo mwezi uliopita kwa mauaji ya wakazi mia moja arobaini na wanane wa jamii ya Kishia katika mji wa Dujail.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yameikosoa hukumu hiyo na yameitaka serikali ya Iraq kutoitekeleza.

Wakili wa Saddam, Khalil Al-Dulaimi, alisema hukumu hiyo itachochea zaidi vita vya kimadhehebu nchini humo.