1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Askari wanne wa Marekani watekwa na kuuawa Iraq.

27 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCXa

Majeshi ya Marekani yamethibitisha askari wanne wa Marekani walitekwa nyara na kuuawa kwenye shambulio la juma lililopita mjini Karbala, kilomita kiasi mia moja na kumi hivi kusini mwa Baghdad.

Wanamgambo waliovalia mavazi ya kijeshi ya Marekani waliokuwa wakizungumza Kiingereza, waliingia kwenye afisi za serikali za mitaa na kuwateka askari hao tarehe 20 mwezi huu.

Kwa mujibu wa msemaji wa majeshi ya Marekani nchini Iraq, wanamgambo hao walikuwa na silaha za kimarekani.

Wakati huo huo, spika wa bunge la Marekani, Bi Nancy Pelosi, aliwasili mjini Baghdad jana kwa ziara ambayo haikutangazwa awali na kushauriana na Waziri Mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki.

Waziri huyo mkuu wa Iraq alimhakikishia Bi Nancy Pelosi kwamba serikali yake imelenga kuusimamia usalama wa nchi hiyo kutoka mikononi mwa majeshi ya Marekani.

Bi Nancy Pelosi alisema anaamini matatizo ya Iraq yanaweza kutanzuliwa tu kwa njia za kisiasa.