1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Makamu wa rais wa zamani amenyongwa

20 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCH6

Makamu wa rais wa zamani wa Irak, Taha Yassin Ramadan, amenyongwa mjini Baghdad hii leo. Ramadan ametiwa kitanzi mwendo wa saa tisa usiku wa kuamkia leo saa za Irak na ni afisa wa nne kunyongwa kuhusiana na mauaji ya Washia 148 katika kijiji cha Dujail mnamo mwaka wa 1982.

Kunyongwa kwake kumefanyika wakati wa maadhimisho ya miaka minne ya vita dhidi ya Irak vilivyoongozwa na Marekani.

Ramadan alihukumiwa kifungo cha maisha jela mwezi Novemba mwaka jana kwa kuhusika katika mauaji hayo, lakini mahakama ya rufaa mjini Baghdad ikaongeza adhabu yake kuwa kifo.

Rais wa zamani wa Irak, Saddam Hussein, na wapambe wake wawili walitiwa kitanzi pia kwa mauaji hayo.

Wakati haya yakiarifiwa watu watano wameuwawa na wengine 17 kujeruhiwa katikati mwa mji mkuu Baghdad wakati bomu lililokuwa limetegwa ndani ya motokaa ililiporipuka karibu na kituo cha polisi.