1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Marekani na Iran zakutana nchini Irak

28 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBxE

Mabalozi wa Marekani na Iran wamefanya mazungumzo ya ngazi ya juu mjini Baghdad kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 27. Mazungumzo hayo yametuwama juu ya machafuko yanayoendelea kuongezeka baina ya Wasunni na Washia nchini Irak.

Balozi wa Marekani nchini humo, Ryan Crocker ameyaeleza mazungumzo baina yake na balozi wa Iran nchini humo, Hassan Kazemi, yaliyodumu kwa muda wa saa nne, kuwa ya kawaida.

Crocker amerudia dai la Marakekani kwamba Iran inawasaidia wapiganaji wa Irak kupambana na vikosi vya Irak na vya Marekani.

´Nimewasilisha mbele ya Wairan baadhi ya maswala yanayotutia wasiwasi kuhusu tabia yao nchini Irak ya kuwasaidia wanamgambo wanaopigana na vikosi vya Irak na vikosi vya jeshi la muungano na kwamba tutakuwa tukitarajia matokeo.´

Iran kwa upande wake imepinga hatua ya Marekani kuikalia Irak na imeishutumu Marekani kwa kuendeleza mtandao wa ujasusi nchini Iran.

Uhusiano wa kidiplomasia baina ya Marekani na Iran ulikatika mnamo mwaka wa 1980 mwaka mmoja baada ya ubalozi wa Marekani mjini Tehran kushambuliwa kwenye mapinduzi ya kiislamu.

Mkutano wa mjini Baghdad umegubikwa na machafuko yaliyozuka mjini humo. Bomu limelipuka karibu na msikiti mkubwa wa Wasunni mjini humo ambapo watu takriban 24 wameuawa na wengine akadhaa kujeruhiwa.