1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Mashambulio ya bomu yameua watu wanane Irak

11 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCtk

Miripuko ya bomu iliyotokea mji mkuu wa Irak Baghdad imeua hadi watu 8 na wengi wengine wamejeruhiwa.Katika shambulio moja bomu liliripuka sokoni Baghdad na shambulio jingine lililenga kombora kwenye ofisi ya mjumbe wa Marekani katika mji wa Hillah kati kati ya Irak. Kwa mujibu wa mwanadiplomasia mmoja,wafanyakazi wa ofisi hiyo hawakujeruhiwa.Wakati huo huo, wizara ya mambo ya ndani ya Irak,imesema mripuko wa bomu umeua mwanajeshi mmoja wa Kipoland na mwengine kutoka Slovakia.Wakati huo huo, majemadari wa Kimarekani wa ngazi ya juu mjini Washington,wanafikiria upya mkakati wa Marekani nchini Irak baada ya chama cha Republikan kushindwa uchaguzi wa bunge na waziri wa ulinzi, Donald Rumsfeld kujiuzulu siku ya Jumatano.Mkuu wa viongozi wa majeshi ya Marekani,Jemadari Peter Pace amedokezea kuwa majemadari wanachunguza upya mkakati wao kuhusu Irak ili wapate kujua wapi marekebisho yanahitaji kufanywa.Kwa upande mwingine kundi la Kituo cha Haki za Kikatiba limesema,litajaribu tena kufungua mashtaka dhidi ya Rumsfeld katika mahakama ya Ujerumani.Mashtaka hayo yanahusika na yale waliotendewa wafungwa katika jela za Abu Ghraib nchini Irak na Guantanamo Bay huko Kuba.Waendesha mashtaka wa Kijerumani mwaka 2004 walikataa kufungua kesi hiyo.