1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Mateka wa Uingereza waendelea kutafutwa

30 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBwX

Mamia ya wanajeshi wa Marekani na Irak wameyafunga maeneo kadhaa ya mtaa wa madongo poromoka wa Sadr mjini Baghdad hii leo na kufanya msako wa kuwatafuta Waingereza watano waliotekwa nyara hapo jana.

Maafisa wa ubalozi wa Uingereza nchini Irak wamefanya mazungumzo na maafisa wa serikali ya Irak kuijadili hali hiyo.

Kamati maalumu ya Uingereza inayolishughulikia swala hilo ilipangiwa kukutana kwa mara ya pili hii leo.

Waziri wa mashauri ya kigeni Uingereza, Margaret Beckett, amesema juhudi zinafanywa kuhakikisha mateka wote wanarejea nyumbani salama salimin.

Sambamba na hayo, Ufaransa leo imelaani vikali utekaji nyara huo wa raia watano wa Uingereza na kutaka waachiliwe huru mara moja.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Ufaransa, Denis Somonneaus, amesema utekaji nyara wa Waingereza hao unadhihirisha kuzorota kwa hali ya usalama ndani ya Irak na kuwatolea mwito raia wa kigeni wasisafiri kwenda nchini humo.

Habari zaidi kutoka Irak zinasema kundi lililo na mafungamano na kundi la kigaidi la al-Qaeda nchini Irak, linalojulikana kwa jina, ´Islamic State of Iraq,´ limedai limeitungua helikopta ya jeshi la Marekani nchini humo.

Jeshi la Marekani lilitangaza hapo awali kwamba helikopta yake moja ilitunguliwa katika mkoa wa Diyala yapata kilomita 57 kaskazini mwa mji mkuu Baghdad hapo jana.