1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD:Kampuni ya Blackwater ya ulinzi kufutiwa kibali

18 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBOt

Iraq inaagiza kufutwa kwa kibali cha kampuni ya huduma za usalama ya Blackwater ya Marekani baada ya kuhusika na mauaji mjini Baghdad yaliyosababisha vifo vya raia 8 na kujeruhi wengine 13.

Kampuni hiyo inayotoa huduma za ulinzi kwa maafisa wa Marekani wanaofanya kazi nchini Iraq aidha inachunguzwa na Marekani yenyewe kuhusiana na tukio hilo.Hii inatokea baada ya maelezo yanayotofautiana kuibuka kuhusu sababu zilizopelekea mauaji hayo.

Kulingana na Marekani na Iraq mauaji hayo yalitokea baada ya bomu kulipuka karibu na msafara wa kidiplomasia wa Marekani katika mtaa wa Al-Yarmuk ulio mjini Baghdad hapo jana.Kulingana na ripoti ya serikali ya Marekani wanamgambo waliojihami kwa silaha walishambulia msafara huo jambo lililosababisha walinzi hao wa Blackwater kufyatua risasi.

Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al Maliki alishtumu kitendo hicho cha walinzi hao huku Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi Condoleeza Rice akijaribu kupoza moto kwa njia za kidiplomasia. Kulingana na afisa mmoja wa kampuni hiyo aliyezungumza na gazeti la TIME msafara wa walinzi wao ulishambuliwa na wanamgambo waliojihami wala sio raia jambo lilisababisha kufyatua risasi ili kujilinda.

Iraq kwa upande wake inasema kuwa wengi ya waliofariki ni wapiti njia.Maafisa wa ubalozi wa Marekani nchini humo bado hawajathibitisha iwapo kibali cha kampuni ya Blackwater kimebatilishwa japo bado wafanyikazi wake hawajafukuzwa.