1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bahrain, UAE zaweka mahusiano ya kidiplomasia na Israel

Daniel Gakuba
16 Septemba 2020

Rais wa Marekani Donald Trump ameongoza sherehe ya kuwekeana uhusiano wa kibalozi kati ya Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain, akiimarisha nafasi ya kuchaguliwa tena mwezi Novemba.

https://p.dw.com/p/3iWs0
USA Washington Weißes Haus | Abkommen Naher Osten
Waziri wa mambo ya nje wa Bahrain, Abdullatif al-Zayani, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, Rais wa Marekani, Donald Trump, na waziri wa mambo ya nje ya UAE, Abdullah bin Zayed al-NahyanPicha: Getty Images/AFP/S. Loeb

 

Akizungumza wakati wa kuyasaini makubaliano hayo katika Ikulu ya White House mjini Washington, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameisifu hatua hiyo, akisema inaweza kuwa mwanzo wa kumaliza kabisa uhasama wa muda mrefu kati ya nchi yake na ulimwengu wa kiarabu.

Amesema ilikuwa siku ya kihistoria inayoashiria mapambazuko mapya ya amani, na kusema hatua ya amani waliyopiga leo, itadumu. Netanyahu ameelezea matumaini yake, kuwa mfano wa Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu utafuatwa na nchi nyingine za kiarabu.

Soma zaidi: Bahrain yaungana na UAE kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Israel 

Waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Abdullah bin Zayed al-Nahyan, binafsi amemsifu Netanyahu, ambaye amesema amechagua amani kwa kusitisha unyakuaji wa ardhi za Wapalestina.

Historia yachukuwa mwelekeo mpya

USA Washington Weißes Haus | Abkommen Naher Osten
Sherehe ya kuyasaini makubaliano hayo imefanyika katika Ikulu ya White House mjini WashingtonPicha: Reuters/T. Brenner

Rais Donald Trump ambaye kusainiwa kwa makubaliano haya ni muhimu kwa sera yake ya nchi za nje huku akielekea katika uchaguzi wa mwezi Novemba, amesema historia ya Mashariki ya Kati imebadilisha mkondo.

''Baada ya miongo ya mgawanyiko na mizozo, tunafikia mapambazuko mapya kwa Mashariki ya Kati. Shukrani kwa viongozi jasiri wa nchi hizi tatu, tunapiga hatua kubwa kuelekea mustakabali ambapo watu wa dini na asili tofauti wataishi pamoja kwa amani na ustawi.'' Amesema Trump.

Soma zaidi: Kwa nini mataifa ya Kiarabu yanakataa mahusiano na Israel

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanasema mafanikio kutokana na makubaliano haya ni madogo, kwa sababu uhusiano kati ya Israel, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu umekuwa mzuri kwa muda mrefu, na nchi tatu hizo zina mtazamo sawa wa kuipinga Iran.

Wapalestina wasema wamesalitiwa

Kwa upande mwingine, Wapalestina wameyapinga makubaliano yaliyosainiwa mjini Washington, wakisema ni usaliti ambao hautasaidia mchakato wa amani.

Mahmud Abbas Kündigt Abkommen mit Israel und USA auf
Kiongozi wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas amesema Bahrain na UAE zimewasiliti WapalestinaPicha: picture-alliance/dpa/A. Badarneh

Kiongozi wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas amesema tatizo lililopo sio kati ya Israel na nchi mbili za kiarabu zilizohusika, bali na Wapalestina ambao ardhi zao zinakaliwa kimabavu.

Saudi Arabia imetoa tangazo la kuwaunga mkono Wapalestina, na kusisitiza kuwa amani ya kudumu itapatikana kwa kuundwa taifa huru la Wapalestina katika mipaka ya mwaka 1967, mji wake mkuu ukiwa Jerusalem Mashariki.

Iran na Uturuki pia ziliyalaani makubaliano hayo hata kabla ya kusainiwa. Spika wa baraza la wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi amesema bunge linahitaji kujua zaidi undani wa makubaliano hayo.

Hayo yakiarifiwa, duru kutoka Ukanda wa Gaza zimearifu kuwa ndege za Israel zimeushambulia ukanda huo, baada ya wanamgambo wa Hamas wanaoudhibiti kurusha kombora lililowajeruhi watu wawili kusini mwa Israel.

 

bk, lc/dr (dpa, AFP, AP)