1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAIDOA: Mapigano makali yaingia siku ya tatu leo

22 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CChF

Katika mapigano makali kuwahi kutokea kufikia wakati huu, wanajeshi wa Somalia wakisaidiwa na wanajeshi wa Ethiopia wamepambana na wapiganaji wa mahakama za kiislamu karibu na makao makuu ya serikali ya mpito ya Somali mjini Baidoa. Pande zote mbili zinadai zimewaua mamia ya watu katika mapigano yaliyoingia siku ya tatu hii leo.

Kiongozi wa mahakama za kiislamu, Sheikh Hasan Dahir Aweys, amewataka wasomali wajiunge na kile alichokiita vita dhidi ya Ethiopia.

Mapigano hayo yamezitatiza juhudi za mjumbe maalumu wa Umoja wa Ulaya, Louis Michel, aliyekuwa amefaulu kuzishawishi pande hizo mbili kurejea katika mazungumzo ya kutafuta amani.

Akizungumza kuhusu mapigano hayo nchini Somalia, Michel amesema machafuko hayatautanzua mgogoro huo. Amesisitiza kwamba njia ya pekee ya kuondokana na mzozo huo ni kuyaanzisha tena mazungumzo ya Khartoum ya kutafuta amani.

Kuna hofu kwamba mapigano hayo huenda yakaenea katika eneo la pembe ya Afrika. Mapigano yalianza Jumanne wiki hii baada ya muda wa wanajeshi wa Ethiopia kuondoka Somalia uliowekwa na wanamgambo wa mahakama za kislamu ulipomalizika.