1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Balozi wa Syria Irak ajiunga na upinzani

12 Julai 2012

Balozi wa Syria nchini Irak amejitenga na serikali na kujiunga na upinzani. Balozi huyo Nawaf Fares (katikati kwenye picha) anatazamiwa kukutana na viongozi wa Irak leo kuzungumza juu ya kupelekwa katika nchi nyingine.

https://p.dw.com/p/15Vkn
Balozi wa Syria mjini Baghdad amejiuzulu
Balozi wa Syria mjini Baghdad amejiuzuluPicha: dapd

Katika ujumbe alioutoa kuhusiana na uamuzi wake wa kujitenga na utawala wa Rais Bashar al-Assad, na ambao umerushwa na kituo cha televisheni cha Al Jazeera, balozi huyo Nawaf Fares amesema pia kuwa amejitenga na chama cha Baath ambacho kiko madarakani nchini Syria, na kuwataka wengine kufuata mfano wake.

''Natangaza kujiuzulu wadhifa wa balozi wa Jamhuri ya Syria nchini Irak, na kutoka chama cha Baath, na nawatolea wito wanachama wengine kufanya hivyo, kwa sababu utawala wa Assad unatutumia kuwanyanyasa wananchi na kuwanyima haki yao ya uhuru na heshima. Natangaza pia kuwa kuanzia sasa naungana na wanamapinduzi wa Syria, kwa sababu huko ndiko ninakopaswa kuwa kwa muda huu na katika mazingira haya.'' Alisema Fares.

Mwanzo wa utawala wa Assad kusambaratika?

General Munaf Tlas pia aliasi jeshi la Syria na kukimbilia Ufaransa
General Munaf Tlas pia aliasi jeshi la Syria na kukimbilia UfaransaPicha: public domain

Hatua hii ya balozi Fares imekaribishwa na Marekani. Msemaji wa Ikulu ya White House, Jay Carney, amesema maafisa wengi wakuu wamekuwa wakimkimbia Rais Assad, iwe katika jeshi na sekta za umma, na kwa maoni ya Marekani, hiyo ni ishara kuwa uungwaji mkono wa utawala wake unasambaratika ndani na nje ya nchi. Bado hakuna tamko lolote kutoka serikali mjini Damascus na Baghdad kuhusu kujitenga kwa Balozi Fares.

Wiki iliyopita, afisa mwenye cheo kikubwa katika jeshi la Syria, Brigedia Jenerali Munaf Tlass pia aliliasi jeshi. Tlass alikuwa akiongoza kikosi maalum cha rais, Republican Guard, na sasa amekimbilia Ufaransa kuungana na baba yake, Mustafa Tlass, aliyewahi kuwa waziri wa ulinzi katika serikali ya baba yake Rais Assad, Hafez al-Assad.

Mivutano ya kidiplomasia

Baraza la Usalama limeshindwa kupata mwafaka juu ya Syria
Baraza la Usalama limeshindwa kupata mwafaka juu ya SyriaPicha: Reuters

Wakati haya yakiarifiwa, harakati za kidiplomasia zinaendelea kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutafuta muafaka juu ya hatua za kuchukuliwa na umoja huo katika mgogoro wa Syria.

Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimewasilisha mswada wa azimio ambalo linatoa muda wa siku kumi kwa rais Assad kutekeleza mpango wa amani wa mpatanishi wa kimataifa kuhusu Syria Kofi Annan, ama sivyo akabiliwe na vikwazo vikali

Lakini Urusi ambayo ni mshirika mkubwa wa serikali ya Syria imeendelea kusimama bega kwa bega na serikali ya rais Assad. Wanachama 15 wa Baraza la Usalama wameshindwa kupata makubaliano ya maana,hata baada ya kutolewa rai ya Kofi Annan, kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya upande wowote utakaokwamisha mpango wake.

Kuondoka kwa balozi Nawaf Fares kunaweza kuwa pigo kubwa kwa rais Bashar al-Assad, ambaye anataka kuonekana kama kiongozi anayepigana vita kuilinda nchi kutokana na makundi yenye silaha yanayosaidiwa na wageni, ambao wanalenga kuipindua serikali.

Kujiuzulu ni pigo kwa Assad

Nchini Syria kwenyewe, wanaharakati wamesema kuwa jeshi la serikali liliendelea kuyashambulia kwa ndege maeneo yanayodhibitiwa na upinzani, huku mapigano ya ardhini pia yakiripotiwa katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef