1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban aitathmini UNAMID huku machafuko yakienea Darfur

Josephat Nyiro Charo10 Machi 2014

Mji wa Saraf Omra katika jimbo la Darfur umeshambuliwa na mali kuibwa huku maelfu ya watu wakifukuzwa kutoka makazi yao mbali na watu 40,000 waliofukuzwa wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/1BMct
Ban Ki-moon New York 27.09.2013 Overlay
Picha: picture alliance/abaca

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, anasema vikwazo vya serikali ya Sudan na vifaa visivyofanya kazi vya baadhi ya wanajeshi wa kulinda amani katika jimbo la Darfur vinakwamisha uwezo wao wa kuwalinda raia na wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada huku machafuko yakizidi kuongezeka katika eneo hilo.

Ban ametoa kauli hizo wakati wa tathmini yake ya tume ya Umoja wa Afrika ya kulinda amani Darfur, UNAMID, ambayo iliamuriwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Julai mwaka jana. Nakala ya ripoti hiyo ilipatikana jana (09.03.2014) na shirika la habari la AFP wakati kukiripotiwa kutokea machafuko makubwa katika eneo hilo katika siku za hivi karibuni.

Katika ripoti hiyo Ban amelitaka baraza la usalama kuridhia hatua kabambe zitakazotekelezwa katika kipindi cha miezi 12 ili UNAMID iweze kuwasaidia vizuri zaidi raia walioathirika na machafuko hayo, ukosefu wa usalama na kunyimwa mahitaji katika jimbo la Darfur.

UNAMID yasuasua kiutendaji

Ripoti ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa inasema huku UNAMID ikiwa imefaulu kuwalinda raia na kutoa mchango katika usambazaji wa misaada, ufanisi wake unakwamishwa na vikwazo vya kuzuiwa kufika maeneo fulani na uwezo mdogo wa vikosi vya jeshi na polisi kutekeleza majukumu yao. Ban amesema hali katika Darfur inabakia ya kutia wasiwasi sana miaka 11 tangu uasi ulipoanza katika eneo hilo.

Ripoti inasema katika miaka miwili iliyopita uchumi wa Sudan unaozorota umesababisha uhalifu kuongezeka na machafuko ya kikabila kutokea na vikosi vya jeshi vimejiunga na mapigano ya kikabila kupigania dhahabu na raslimali nyingine. Ban anasema kuchelewa kwa serikali ya Sudan kuruhusu bidhaa kwa ajili ya UNAMID kuingia nchini humo kumeikwamisha tume hiyo, ingawa visa kwa ajili ya wafanyakazi wa tume hiyo zimekuwa zikitolewa haraka katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Wanajeshi wa UNAMID katika jimbo la Darfur, Sudan
Picha: Reuters

Ban amegusia mapungufu ya vifaa vya walinda amani, mafunzo na utayarifu wao akisema vinawazuia wanajeshi kufanya kazi barabara na kupunguza uwezo wao kuzuia mashambulizi. Kiongozi huyo ameihimiza tume ya UNAMID iyape kipaumbele mambo matatu - kuwalinda raia, kusaidia shughuli za utoaji misaada na kusaidia juhudi za upatanishi katika mizozo ya jamii ya Darfur.

Machafuko yaenea Darfur

Wakati haya yakiarifiwa, UNAMID imeripoti jana kuwa machafuko yameenea katika jimbo la Darfur, huku wizi ukifanyika na watu wakipoteza makazi yao. Katika taarifa yake UNAMID imesema maelfu ya watu wamelazimika kuukimbia mji wa Saraf Omra, kiasi kilometa 100 mashariki mwa mji wa El-Geneina, mji mkuu wa jimbo la Darfur Magharibi. Wengi wao wametafuta hifadhi katika kambi ya UNAMID katika eneo hilo na tume hiyo inawalinda na kuwapa maji walioathiriwa pamoja na matibabu kwa watu zaidi ya 30 waliojeruhiwa.

Doria zilizofanywa na UNAMID zimebaini kuwa wizi wa mali umefanyika mjini humo na eneo la soko limeharibiwa katika kile inachosema ni machafuko ya kikabila.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE

Mhariri: Daniel Gakuba