1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban Ki-moon aanza ziara Maziwa Makuu

Admin.WagnerD22 Mei 2013

Benki Kuu ya Dunia itatoa dola bilioni 1 kusaidia maendeleo ya eneo la maziwa makuu. Rais wa Benki hiyo Jim Yong Kim ameyasema hayo mjini Kinshasa alikowasili akiandamana na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki moon

https://p.dw.com/p/18bxf
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moonPicha: Reuters

Akizungumza mjini Kinshasa, Rais wa Benki Kuu ya Dunia Jim Yong Kim amesema kuwa fedha hizo zitakazotolewa na benki anayoiongoza zitatumika kuboresha huduma za afya na elimu, miradi ya kuzalisha umeme kutumia nguvu ya maji, na biashara katika mipaka ya nchi za maziwa makuu. Jim amesema na hapa namnukuu, ''Tunaamini kuwa fedha hizi zitatoa mchango mkubwa katika mchakato wa keleta amani ya kudumu katika eneo la Maziwa makuu''. Mwisho wa kumnukuu. Rais huyo wa Benki Kuu ya Dunia ameongeza kuwa fedha hizo zitasaidia kuinua shughuli za kiuchumi, kuunda nafasi za ajira, na kuinua kiwango cha maisha ya watu wa eneo hilo ambao wameteseka kwa muda mrefu.

Rais wa Benki Kuu ya Dunia Jim Yong Kim anaambatana na Ban Ki-moon katika ziara ya Maziwa Makuu.
Rais wa Benki Kuu ya Dunia Jim Yong Kim anaambatana na Ban Ki-moon katika ziara ya Maziwa Makuu.Picha: REUTERS

Wakiwa mjini Kinshasa leo, viongozi hao watafanya mazungumzo na Rais Joseph Kabila, na pia watakutana na viongozi wengine wakuu wa nchi hiyo, wakiwemo Spika wa Bunge na Rais wa Seneti, na wakuu wa mashirika ya kiraia.

Vita vyatokota mashariki

Ziara ya viongozi hao katika eneo la maziwa makuu imekuja wakati kukiwa na makabiliano mapya baina ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa M23. Jana, serikali ya Kongo ilisema kuwa watu 19 wamekwishauawa katika mapigano yanayoendelea karibu na mji wa Goma, mashariki mwa nchi hiyo.

Mapigano hayo ni ya kwanza kutokea tangu Novemba mwaka jana, ambapo waasi wa M23 walilizidi nguvu jeshi la serikali na kuuteka mji wa Goma ambao ndio makao makuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini, ingawa mji huo ulikuwa ukilindwa na maelfu ya wanajeshi kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Nchi jirani ya Rwanda imeshutumiwa na tume ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa pamoja na serikali ya Kinshasa kuwa inawaunga mkono waasi wa M23, lakini nchi hiyo imezikanusha shutuma hizo.

Juhudi za kusaka amani zaendelea

Mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa M23 ambayo yalifanyika mjini Kampala yamekwama. Wengi wa wapiganaji wanaoliunda kundi la M23 ni kutoka jamii ya watutsi kutoka kundi jingine la waasi, ambalo lilijumuishwa katika jeshi la serikali baada ya mkataba wa amani uliosainiwa mwaka 2009.

Eneo la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekabiliwa na vita kwa karibu miongo miwili.
Eneo la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekabiliwa na vita kwa karibu miongo miwili.

Hata hivyo wengi wao waliliasi tena jeshi mwaka jana, na wameanzisha mazoezi katika maeneo wanayoyadhibiti, wakijiandaa kukabiliana na kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa, ambacho kinatumwa kuyamaliza makundi ya waasi yaliyoenea katika sehemu hiyo.

Alipokuwa akizungumza jana katika mji mkuu wa Msumbiji, Maputo kabla ya kuelekea Kinshasa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alisema kikosi hicho hakina budi kutumwa haraka kuanza kutekeleza majukumu yake, kwa kuzingatia hali halisi ya mambo ilivyo sasa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/DPAE

Mhariri:Yusuf Saumu