1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban Ki-Moon asifu maendeleo yaliyopatikana Iraq

P.Martin29 Mei 2008

Iraq,kwenye mkutano wa kimataifa mjini Stockholm,kwa mara nyingine tena imetoa wito wa kusamehewa madeni ya kama Dola bilioni 60 na kuondolewa vikwazo vilivyowekwa wakati wa utawala wa Saddam Hussein.

https://p.dw.com/p/E910

Kwa kweli mkutano wa Stockholm umeitishwa kutathmini maendeleo yaliyopatikana kuambatana na mradi wa miaka mitano unaohusika na ujenzi mpya wa Iraq na sio kujadili suala la kufutiwa madeni.Hata hivyo Waziri Mkuu wa Iraq Nouri al Maliki alitoa wito huo kwa wajumbe wa serikali na mashirika mbali mbali waliohudhuria mkutano huo wa siku moja.Alisisitiza vipi madeni na vikwazo vilivyowekwa enzi ya Saddam Hussein,vinavyozuia maendeleo na ujenzi mpya wa nchi.

Kwa mfano amesema,Iraq inailipa Kuwait mabilioni ya Dola kufidia hasara iliyosababishwa na uvamizi wa Saddam Hussein mwaka 1990.Si hilo tu kwani Baghdad inapaswa pia kulipa asilimia 5 ya pato lake la mafuta katika mfuko wa Umoja wa Mataifa kufidia hasara zilizosababishwa vitani.Sehemu kubwa ya deni hilo inahusika na vita vya Iraq na Iran vilivyopiganwa kati ya mwaka 1980 na 1988.

Waziri Mkuu al-Maliki amesema,Iraq inahitaji kuondolewa mzigo huo - na kuongezea kuwa licha ya hayo yote Iraq imefanikiwa kupiga hatua kubwa kuleta utulivu wa kudumu katika maeneo yote.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon katika hotuba yake ya ufunguzi aliisifu serikali ya Iraq kwa maendeleo yanayodhihirika katika sekta za usalama,uchumi na siasa.Maendeleo hayo yametimiza malengo yaliyopangwa mwaka jana kwenye mkutano wa Sharm el-Sheikh nchini Misri.Akaongezea:

"Vile vile tumeshuhudia dhamira mpya ya kuimarisha utawala wa kisheria.Kwa juhudi hizo,Iraq inajitoa kwenye janga tulilohofia sana."

Ingawa hali ya usalama imeboreshwa nchini Iraq, maendeleo ya kisiasa yanakwenda pole pole tangu nchi hiyo kuvamiwa na Marekani mwaka 2003.Juhudi za upatanisho wa kitaifa zinakwama kwa sababu ya mivutano ya kimadhehebu kati ya makundi ya Kishia na Kisunni.

Hata hivyo Waziri Mkuu al-Maliki amesema,serikali yake inatazamia kuwa na uchaguzi wa majimbo katika mwezi wa Oktoba.

Kwa maoni ya Washington uchaguzi ni hatua iliyo muhimu sana,katika jitahada ya kuwajumuisha Wairaki wa madhehebu ya Sunni walio wachache,katika utaratibu wa kisiasa na hivyo kupunguza mivutano ya kimadhehebu iliyoitumbukiza nchi hiyo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2006.Iran iliyohudhuria mkutano wa Stockholm imesema ipo tayari kutoa mchango mkubwa katika ujenzi mpya wa Iraq.