1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bara Ulaya lashuhudia viwango vya juu vya joto

Admin.WagnerD25 Julai 2019

Paris, London na miji mingine mikubwa barani Ulaya inakabiliwa na viwango vya juu vya joto vinavyokaribia kuvunja rekodi hii leo.

https://p.dw.com/p/3MjYW
Frankreich, Auzances: Dürre durch Hitzewelle
Picha: Reuters/R. Duvignau

Wataalamu wa hali ya hewa wanaonya kuwa huenda hali hii ikawa ya kawaida katika sehemu nyingi za dunia. Lakini barani Ulaya ambapo matumizi ya viyoyozi ni ya kiwango cha chini, hawakujiandaa kwa viwango hivyo vya joto na kusababisha joto kali wiki hii.

Kwa hivyo watalii wamekimbilia katika maeneo ya chemi chemi za maji na maafisa wa serikali pamoja na wale wakujitolea wakiwapepea wazee , wagonjwa na wasiokuwa na makao walioathirika zaidi na joto hilo.

Safari za treni zimefutiliwa mbali nchini Uingereza na Ufaransa na maafisa wa serikali nchini Ufaransa wamewahimiza wasafiri kutulia nyumbani. Rekodi za joto zinavunjwa moja baada ya nyingine barani Ulaya. Hii leo mchana viwango vya joto mjini Paris vilifikia nyuzi 40.6 na kuvunja rekodi ya awali ya nyuzi 40.4 mnamo mwaka 1947.

Maafisa wa serikali wanasema kuwa viwango hivyo bado vitaongezeka kutokana na upepo mkavu na moto kutoka eneo la Afrika Kaskazini ambapo limo katikati ya mifumo baridi yenye dhoruba.

Mji wa London unatarajiwa kuwa na viwango vya nyuzi 39 na maeneo ya Ujerumani ,Uholanzi, Luxembourg na uswisi huenda yakawa na viwango vya joto vinavyopita nyuzi 40.

Nchini Ubelgiji, idara ya utabiri wa hali ya hewa inasema kuwa taifa hilo limeshuhudia viwango vya joto vya nyuzi zaidi ya 40 kwa mara ya kwanza tangu rekodi zianze kuwekwa . Viwango vya sasa ni nyuzi 40.2.

Nchini Ujerumani, hapo jana ilirekodi viwango vya joto vya nyuzi 40.5 na idara ya utabiri wa hali ya hewa ya Ujerumani imethibitisha kiwango cha juu kabisaa cha joto kuwahi kurekodiwa Ujerumani cha nyuzijoto 41.5.

Nchini Austria mtoto wa miaka miwili amefariki kutokana na ukosefu wa maji mwilini katika eneo la Styria baada ya kupanda, kusinzia na hatimaye kulala juu ya gari lililokuwa limeegeshwa na kupata joto kupita kiasi . Haya ni kulingana na kituo cha habari cha Austria.

Katika baadhi ya maeneo ya Ujerumani, Uswisi na Austria, baadhi ya jamii zilipaka barabara za reli rangi nyeupe na kutarajia kuwa rangi hiyo huenda ikapunguza viwango vya joto kwa nyuzi chache .

Katika miji ya London na Paris, maafisa wa serikali na wafanyakazi wa msaada waliwapa maji watu wasiokuwa na makao na kufungua  vituo vyakuwawezesha kuoga na kupumzika.

Huku joto hilo likiendelea kukithiri, wanasayansi wanasema kutakuwa na vipindi zaidi vya joto ambalo litaongezeka kuwa kali kama viwango vinavyoikumba Marekani ijapokuwa ni mapema sana kujuwa iwapo joto hili linahusiana na mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na shughuli za kibinadamu.