1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barack Obama afungua ukurasa mpya katika historia ya Marekani

C.Schmiester/P.Martin4 Juni 2008

Seneta Barack Obama ametangaza ushindi wake katika kinyangányiro cha kuwania kuteuliwa mgombea uchaguzi wa rais kwa tikti ya chama cha Demokratik na hivyo kufungua ukurasa mpya katika historia ya Marekani.

https://p.dw.com/p/EDOU
Democratic presidential hopeful, Sen. Barack Obama, D-Ill., speaks during a primary election night rally in St Paul, Minn., Tuesday, June 3, 2008. Obama claimed the Democratic presidential nomination Tuesday night in a long-time-coming victory speech that minced no words about his opponent in the fall campaign, Republican John McCain. (AP Photo/Chris Carlson)
Seneta Barack Obama wa chama cha Demokratik anatazamia kugombea uchaguzi wa rais wa Marekani Novemba 2008.Picha: AP

Katika hotuba yake mbele ya umati uliokuwa ukimshangilia alisema:

"Kwa sababu yenu,usiku wa leo ninaweza kusimama hapa na kusema,mimi nitakuwa mgombea wa chama cha Demokratik katika uchaguzi wa rais wa Marekani."

Kwa hivyo Barack Obama ambae baba yake ni Mkenya na mama ni Mmarekani Mzungu,atakuwa Mmarekani wa kwanza mwenye asili ya Kiafrika kugombea urais nchini Marekani na hivyo kufungua ukurasa mpya katika historia ya nchi hiyo.Katika uchaguzi wa awali uliofanywa Jumanne katika majimbo ya South Dakota na Montana,Obama mwenye miaka 46 alifanikiwa kujinyakulia jumla ya kura 2,156 za wajumbe na hivyo kupindukia kiwango cha 2,118 kinachohitajiwa ili kuweza kuteuliwa rasmi katika mkutano mkuu wa chama utakaofanywa mwezi Agosti.

Alipotoa hotuba yake St.Paul, Minnesota Obama alishangiliwa na umati wa 17,000 uliokusanyika ndani ya ukumbi na wengine 15,000 waliokuwa nje.Katika hotuba ya kusisimua,Obama alitoa wito wa kufanywa mageuzi ya kisiaasa.Akaongezea:

"Daima kila kizazi kilichokabiliwa na changamoto kali, kiliwaachia watoto wake ulimwengu ulio bora na wenye imani na haki zaidi.Na sasa ni wakati wetu kufungua ukurasa mpya,kupambana na changamoto zinazotukabili.Njia hiyo itakuwa ngumu na ndefu."

Juu ya hivyo amesema,ni imani yake kuwa chama cha Demokratik kitakuwa na msimamo mmoja kabla ya kufanywa uchaguzi wa rais Novemba ijayo.Akamsifu Clinton alietazamia kuwa rais wa kike wa kwanza nchini Marekani.

Amesema,katika kampeni hii Clinton amefungua ukurasa mpya katika historia ya Marekani,si kwa sababu ya kuwa mwanamke wa kwanza kufanya kile ambacho hakijawahi kufanywa na mwanamke mwengine hapo awali,bali sababu ni kwamba yeye ni kiongozi anaewapa matumaini mamilioni ya Wamarekani.

Lakini Seneta Hillary Clinton mwenye miaka 60, alieshindwa kufikia kiwango cha 2118 kinachohitajiwa, hajakiri kushindwa.Mjini New York alipowahotubia wafuasi wake alisema:

"Hii ilikuwa kampeni ndefu.Na sitopitisha maamuzi yo yote usiku wa leo."

Lakini wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanazungumzia uwezekano wa Clinton kugombea wadhifa wa makamu wa rais.Inasemekana kuwa Obama alipozungumza kwa simu na Clinton kumpongeza kwa ushindi wake katika jimbo la South Dakota,alimuambia Clinton angependa kukutana nae hivi karibuni.

Obama katika uchaguzi wa rais uliopangwa kufanywa Novemba mwaka huu atapambana na John McCain wa chama cha Republikan.