1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barack Obama-Siku 100 za mwanzo madarakani

29 Aprili 2009

Ni siku 100 tangu Barack Obama kuapishwa rais mpya wa Marekani . Na kama ilivyo desturi,ni wakati wa kuchunguza yale yaliyotimizwa na rais mpya katika kipindi hicho.

https://p.dw.com/p/Hgez
Symbolbild 100 Tage Obama Präsident der USA
Rais wa Marekani Barack Obama.Picha: AP/DW-Montage

Kampeni yake ya uchaguzi imetoa matumaini ya kutaraji enzi mpya. Je, kwa umbali gani Obama amefanikiwa kutekeleza ahadi zake? Siku 100 za mwanzo madarakani zilikuwa rahisi kwa Barack Obama.Kwani kwanza kabisa alipaswa kutenda moja: yaani kujitofautisha na mtangulizi wake na siasa zake. Hiyo haikuwa changamoto kubwa hivyo.Kwani uchunguzi wa maoni uliofanywa kuhusu George W.Bush alipokuwa akiondoka madarakani, ulionyesha kuwa kiongozi huyo alipoteza umaarufu wake kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa nchini Marekani kuhusu rais anaemaliza muhula wake.Hata jumuiya ya kimataifa ilikuwa na hamu kubwa kuona rais mpya nchini Marekani mradi si Bush.

Barack Obama alizicheza vizuri karata zake.Kwani muda mfupi tu baada ya kushika madaraka,alitoa amri ya kuifunga jela ya Marekani Guantanamo, akapiga marufuku wafungwa kuteswa,akaamua kuviondosha vikosi vya Marekani kutoka Iraq,akainyoshea mkono Urusi kuanzisha upya majadiliano,akawasilisha mpango wa kufufua uchumi kwa kuwekeza katika sekta za elimu na afya na alitangaza sera mpya za nishati. Orodha ni ndefu mno. Ni dhahiri kuwa Obama ana kipaji pekee cha kuweza kutekeleza mambo mengi kwa wakati mmoja.Lakini pia ameonyesha udhaifu wa hapa na pale. Kwa mfano kuhusu suala iwapo tume ya uchunguzi ijishughulishe na ripoti zilizowekwa na serikali ya Bush kuhusu mateso ya wafungwa. Hadi hivi sasa pia hajafanikiwa kushirikiana na chama cha upinzani cha Republikan kinyume na vile alivyotangaza hapo awali.Lakini kwa jumla, anafuata msimamo wake ule ule wa awali.Licha ya umri wake mdogo na kutokuwa na uzoefu,Barack Obama tangu alipokabidhiwa wadhifa wa urais ameonyesha kuwa anaiweza kazi hiyo.

Na raia wa Marekani wanaendelea kumuamini rais wao.Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti la Washington Post,takriban asilimia 60 ya watu walioulizwa maoni yao wamesema kuwa wameridhika na jinsi Obama anavyoitekeleza kazi yake.Katika kipindi cha siku 100 za mwanzo,Rais Obama ametimiza ahadi yake ya kufuata siasa zilizo tofauti na zile za mtangulizi wake.

Mwandishi:C.Bergmann

Mhariri:Abdul-Rahman