1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza kuu la Umoja wa mataifa kulijadili takwa la Serbia kuhusuTangazo la uhuru la Kosovo.

7 Oktoba 2008

Serbia yataka mahakama ya kimataifa itowe uamuzi wa kisheria.

https://p.dw.com/p/FVf7
Sherehe za katiba mpya ya Kosovo bungeni mjini Pristina Juni 15,2008.Picha: AP

Mvutano baina ya Serbia na Jimbo liliojitenga la Kosovo unazidi kupamba moto kabla ya kikao cha baraza kuu la umoja wa mataifa hii leo, wakati wanachama watakapoamua iwapo waliridhie takwa la Serbia kuomba mahakama ya sheria ya kimataifa mjini The Hague iamue juu ya suala hilo. Lakini tayari hilo limepingwa na Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Kosovo.

Waziri huyo wa mashauri ya kigeni wa Kosovo Skender Hyseni amesema suala la nchi kuwa huru si la mahakama bali ni la uamuzi wa kisiasa wa viongozi wa kisiasa.

Serikali ya Serbia inataka mahakama ya sheria ya kimataifa yenye makao makuu mjini The Hague itoe ushauri juu ya haki ya kisheria ya tangazo la uhuru wa Kosovo la Februari 17 mwaka huu. Ombi kama hilo linahitaji kuidhinishwa na baraza kuu la Umoja wa mataifa.

Alipohutubia kwenye Umoja wa mataifa Septemba 23, Rais wa Serbia Boris Tadic alieleza wazi madai ya Serbia kuwa Kosovo ni ardhi yake na akazitaka nchi wanachama ziunge mkono suala hilo liamuliwe na mahakama ya sheria ya kimataifa.

Pamoja na kutambua kwamba omb la Serbia huenda likapitishwa, hata hivyo waziri wa mashauri ya kigeni wa Kosovo alionekana kujiamini kwamba hatimae ombi hilo halitozusha kikwazo cha aina yoyote katika hatua ya Kosovo kujitangazia uhuru au ya kutambuliwa na mataifa mengine.

Pamoja na hayo katika kipindi kifupi, ni jambo linaloweza kuchelewesha juhudi za Kosovo kujiunga na Jumuiya na za kimkoa na kimataifa-kama Umoja wa mataifa, Benki ya dunia na Shirika la fedha la kimataifa IMF. Halikadhalika linaweza kuathiri msimamo wa baadhi ya nchi kuhusiana na kuitambua Kosvo kama dola huru. Uingereza iliunga mkono msimamo wa Kosovo, ikisema " Umoja wa mataifa hauna wasi wasi juu ya haki ya kisheria ya tangazo la uhuru wa Kosovo."

Uhuru wa Kosovo unaungwa mkono na nchi 42 kati ya 192 wanachama wa Umoja wa mataifa. Wakati nchi za ulaya magharibi, Uturuki na Marekani zilikua za kwanza kulikubali tangazo la uhuru wa Kosovo, ni nchi moja tu miongoni mwa majirani wanne wa Karibu wa Kosovo iliyoitambua-nayo ni Albania.Hata hivyo kulikua na ishara wiki iliopita kuwa Montenegro na Macedonia zinakaribia kuitambua Kosovo.

Licha ya tangazo lake la Uhuru, Kosovo bado iko katika mamlaka ya usimamizi wa Umoja wa mataifa, tangu Jumuiya ya kujihami ya NATO ilipoihujumu Yugoslavia kwa mabomu 1999, kusitisha zoezi la kijeshi la safisha safisha ya kikabila huko Kosovo, lililoendeshwa na utawala wa zamani wa Slobodan Milosevic katika Yugoslavia ya zamani, Mivutano imeongezeka huko Kosovo tangu wakati huo kati ya waliowengi ambao ni wenye asili ya Kialbania na wachache wa asili ya Serbia.

Serbia imependekeza suluhisho, ikitaka eneo la kaskazini mwa Kosovo , sehemu pekee ya wakaazi wengi wa Kiserbia liwe la Serbia ikiwa na maana kuchorwa mpaka mpya. Lakini Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Kosovo Hyseni amelikataa wazo hilo akisema wapinga hatua yoyote ya kuabdili mipaka yake na akaonya kwamba itakua sawa na kuzusha ugomvi na mgogoro mwengine. Akasema tayari bunge la Kosovo limepitisha sheria kulinda haki za wachache wenye asili ya Serbia katika sekta kama elimu, afya na kuyatawanya mamlaka ya kiutawala.