1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lapitisha azimio la haki za watu wa makabila asilia.

Mohamed Dahman14 Septemba 2007

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeidhinisha kwa kauli moja azimio la haki za watu wa makabila asilia hapo jana licha ya upinzani kutoka nchi kadhaa zilizoendelea ambazo zimesema limetowa madaraka makubwa ya kisheria na udhibiti wa mali kwa watu hao wa makabila asilia.

https://p.dw.com/p/CHjH

Nchi nne za Canada,Marekani Australia na New Zealand zimepiga kura dhidi ya waraka huo usiobana kisheria lakini ulipitishwa kwa kauli kubwa kwa kura 143 za kuunga mkono na nchi 11 hazikushiriki kupiga kura.Sio nchi zte 192 katika Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa zimeshiriki kupiga kura hiyo.

Baada ya kujadiliwa kwa miakia 20 waraka wa azimio hilo unasema kwamba watu wa kabila asilia ambao idadi yao milioni 270 duniani kote kama wanvyofahamika na azimio hilo wana haki ya kujiamulia mamabo yao wenyewe.

Mojawapo ya kipengele kilichozusha utata mkubwa kinataja kwamba watu wa makabila asilia wana haki ya kumilki ardhi, maeneo na rasilmali ambazo wamekuwa wakizimiliki tokea enzi na dahari au wamezikalia,kuziztumia au kujipatia.

Kipengele hicho kinaweza kuhoji umiliki wa takriban ardhi yote katika nchi kama zile ambazo zimelipiga azimio hilo ambazo idadi ya watu wake hivi sasa kwa kiasi kikubwa nasaba yao inatokana na walowezi ambao wamechukuwa maeneo hayo kutoka kwa watu waliokuweko kabla yao.

Kipengele kilichowekewa uwiano kilichoingizwa dakika za mwisho kwenye maudhui ya azimiho hilo kinasema hakuna kitu kinachoweza kuamrisha au kushajiisha hatua yoyote ile ambayo itagawa au kudhoofisha kwa ujumla au kwa sehemu fulani uhuru wa mipaka ya maeneo au umoja wa kisiasa.

Lakini halikuwatosheleza sana wale walilolipiga hususan Canada ambapo suala hilo limekuwa kabumbu la kisiasa. Waaborigin wengi wa Canada takriban milioni moja na watu wa kabila la Inuit wanaishi kwenye nyumba ziliojaa watu kupindukia zisizo safi na hakabiliwa na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira, kudhulumiwa na kujiua wenyewe.

Balozi wa Canada katika Umoja wa Mataifa John McNee ameliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba vifungu kwenye azimio hilo kuhusu ardhi, maeneo na rasilmali vimelezwa kwa mapana mno, haviko wazi na vinaweza kutafsiriwa kwa dhana tafauti.

Mjumbe wa Marekani Robert Hagen amesema Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa lililoandaa madhui ya azimio hilo halikutafuta muafaka na kwamba azimio hilo limepitishwa kwa kura iliogawika na ameuita mchakato huo kuwa wa bahati mbaya na usio wa kawaida.

Mbali ya masuala yanayohusu ardhi wakosoaji pia wanashambulia vipingele kuhusu haki miliki ya watu wa makabiloa asilia,haki ya kushauriwa juu ya sheria zinazowagusa na haki ya kutoziingiza ardhi zao katika shughuli za kijeshi.

Lakini wanaoliunga mkono azimio hilo wanasema limetowa utambuzi uliochelewa mno wa haki za watu wa makabila asilia.

Waziri Mkuu wa Bolivia David Choquhuanca ambaye yeye mwenyewe binafsi ni wa kabilia asilia ameliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa kupitishwa kwa azimio hilo ni hatua muhimu kwa watu wa makabila asilia kuondokana na ubaguzi, kuimarisha utambulisho wao, kutambuliwa kwa haki zao kwa ardhi na mali asili, kushauriwa na kushiriki katika kufanya maamuzi.

Takriban washirika wote wa Marekani wakiwemo Uinge´gereza na Japani pia zimesaini azimio hilo kwa kusema kwamba marekebisho ya dakika za mwisho yamelifanya liwe linakubalika na kwa kuzingatia kwamba halina nguvu ya kuwa sheria ya kimataifa.