1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la haki za binadamu lapata wajumbe wapya

13 Novemba 2013

Mataifa manne yanayoshutumiwa kuwa na rekodi mbaya ya haki za binaadamu, yameshinda viti katika Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa, kwa miaka mitatu.

https://p.dw.com/p/1AGHK
Wajumbe wa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa wakiwa mkutanoni
Wajumbe wa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa wakiwa mkutanoniPicha: Reuters

Uchaguzi huo umefanyika licha ya kuwepo wasiwasi kuhusu ukiukwaji wa haki za binaadamu na vikwazo juu ya uhuru kwenye nchi hizo.

Mataifa hayo China, Cuba, Urusi na Saudi Arabia, ni miongoni mwa mengine 14 yaliyojishindia viti hivyo katika uchaguzi wa mwaka, baada ya kupata theluthi moja ya kura za wajumbe wa baraza hilo lenye makao yake mjini Geneva.

Nchi nyingine zilizojipatia viti katika baraza hilo lenye wanachama 47, ni pamoja na Algeria, Uingereza, Ufaransa, Mexico, Maldives, Morocco, Namibia, Afrika Kusini, Vietnam na Macedonia.

Balozi wa Marekani UN, Samantha Power
Balozi wa Marekani UN, Samantha PowerPicha: Reuters

Nchi hizo zimechaguliwa jana Jumanne (12.11.2013) na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 193, huku balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Samantha Power akielezea wasiwasi wake kuhusu uteuzi wa baadhi ya nchi.

Makundi ya kutetea haki za binaadamu yamepinga uteuzi wa mataifa hayo.

Baraza hilo lakabiliwa na changamoto

Mkurugenzi Mtetezi wa kimataifa wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, Peggy Hicks, amesema kuwa wanachama hao wanne wapya pamoja na Algeria, walikataa kuwaruhusu wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kuzuru kwenye nchi hizo kuchunguza madai ya kuwepo unyanyasaji na ukiukwaji wa haki.

Hicks amesema wanachama wa baraza hilo itabidi wafanye juhudi zaidi kuhakikisha wanakabiliana na changamoto kadhaa.

Kwa mujibu wa shirika la utetezi la Umoja wa Mataifa, linaloufuatilia umoja huo, ni nchi nne tu kati ya wagombea 16 waliokuwa wanawania viti hivyo 14, ndizo zilizokuwa na sifa ya kuwa wanachama wa baraza hilo la haki za binaadamu. Nchi hizo ni Uingereza, Ufaransa, Macedonia na Mexico.

Nembo ya Human Rights Watch
Nembo ya Human Rights Watch

Mataifa mapya yaliyochaguliwa, yataanza kazi rasmi kuanzia mwaka 2014 hadi 2016. Iran na Syria zilikuwa zinapanga kuwania nafasi hiyo, lakini zilijiondoa baada ya kukosolewa kutokana na rekodi yao ya haki za binaadamu.

Jordan yajiondoa kuipa nafasi Saudi Arabia

Hadi wiki iliyopita, Jordan ilikuwa inagombea kiti hicho, lakini ikajiondoa ili kuiruhusu Saudi Arabia igombee bila ya kuwa na mpinzani.

Jordan inataka kuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua nafasi iliyoachwa na Saudi Arabia, ambayo ilikataa kiti hicho kuanzia mwaka 2014 hadi 2015, mwezi uliopita.

Mfalme Abdullah II Bin Al Hussein wa Jordan
Mfalme Abdullah II Bin Al Hussein wa JordanPicha: Getty Images/Andrew Burton

Tangu kuundwa kwake, Baraza la Haki za Binadaamu la Umoja wa Mataifa limekuwa likikabiliwa na changamoto kadhaa, huku kazi ya kuzifuatilia nchi wanachama ikiwa ni jukumu gumu.

Aidha, Bibi Power amesema uchaguzi huo unakumbusha kwamba kazi muhimu ya baraza hilo bado haijakamilika.

Nchi zilizoangushwa katika uchaguzi huo ni Uruguay, iliyoshindwa na Cuba na Mexico katika viti vya Amerika ya Kusini na kundi la Caribbean, pamoja na Sudan Kusini ambayo ilishindwa kupata kura za kutosha ili kushinda kiti kimoja kati ya vinne vya Afrika.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,APE
Mhariri: Daniel Gakuba