1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Mataifa: Mtoto wa vita vya kwanza vya dunia aliesahaulika

Admin.WagnerD4 Juni 2014

Mauaji yaliyotokea wakati wa vita vikuu vya kwanza vya dunia yalizaa azma la kutoruhusu tena mgogoro kama huo kutokea. Baraza la Mataifa, ambalo lilikuwa wazo la rais wa Marekani, lilijaribu kutoa jukwa la kutimiza hilo.

https://p.dw.com/p/1CCJc
Krieg der Propaganda USA
Picha: picture alliance/akg-images

Lakini wakati baraza hilo lilishindwa kuzuwia vita vikuu vya pili vya dunia miaka 20 baadaye, lilitoa funzo kwa walioanzisha Umoja wa Mataifa baada ya vita vikuu vya pili vya dunia.

Vita vya kwanza vya dunia viliisha kwa mikataba kadhaa ya kusitisha mapigano, ukiwemo uliyosainia na Ujerumani Novemba mwaka 1918, na kukamilishwa katika mji wa Versailles Julai 1919. Kukiwa na wanajeshi na raia wasiopungua milioni 16 waliouawa katika vita hivyo hivyo, hali ilikuwa ni ya kutisha.

Wapatanishi walianzisha Baraza la Mataifa kama jaribio kubwa la kutatua migogoro kwa njia za mani. Tatizo kubwa lilikuwa kwamba kila mmoja ya mataifa 58 wanachama wa Baraza hilo lilikuwa na kura ya turufu.

Propaganda ya washirika wa Ujerumani na Austria wakati wa vita vikuu vya kwanza vya Dunia.
Propaganda ya washirika wa Ujerumani na Austria wakati wa vita vikuu vya kwanza vya Dunia.Picha: picture-alliance/akg-images

Tatizo lingine ni kwamba maamuzi ya Baraza la Mataifa hayakuwa yanayafunga mataifa kuyatekeleza na baraza hilo halikuw ana meno kama vile kuweka vikwazo. Maamuzi ya sasa ya baraza la usalama yana uhalali wa kisheria.

Na kubwa zaidi lilikuwa kukataa kwa bunge la Marekani kuridhia uanachama wa Baraza hilo ambalo majadiliano ya kulianzisha yalioongozwa na rais wa Marekani wakati huo Woodrow Wilson. Hii leo, Marekani ndiye mchangiaji mkubwa zaidi kwa shirika lililochukuwa nafasi ya Baraza la Mataifa.

Kushindwa kwa Baraza la Mataifa

Katika miaka 1920, Baraza lilikuwa na mafanikio kadhaa, likifanya upatanishi katika migogoro ya mipaka kati ya Finland na Sweden, Yugoslavia na Albania, na Hungary na Jamhuri ya Czeck kwa mfano. Lakini katika muongo mmoja kuelekea vita vya pili vya dunia, baraza hilo lilishindwa kuiwekea vikwazo Japan ilipoivamia Manchuaria mwaka 1931, au pale Italia ilipoivamia Abyssinia, au kuingilia kati katika vita vya Uhispania kati ya mwaka 1936 hadi 39.

Kufikia mwaka 1939, Baraza la Mataifa lilikuwa haliwezi kuzizuwia Ujerumani, Italia au Japan, ambazo zilikuwa zimejiondoa na kuwa washirika katika vita vikuu vya pili vya dunia. Hata hivyo Baraza hilo liliusimamisha uanachama, muungano wa Kisoviet mwaka 1939 kutokana na kuivamia Finland.

Stephen Schesinger, mwandishi wa kitabu cha Act of Creation, kinachozungumzia uanzishwaji wa Umoja wa Mataifa, aliliambia shirika la habari la Ujerumani dpa, kuwa haoni kama Baraza la Mataifa linastahili kutambuliwa wakati huu isipokuwa tu kutokana na ukweli kwamba liliwakilisha hatua ya kwanza ya kimataifa kuelekea kuundwa kwa Umoja wa Mataifa.

Viongozi wa kisiasa na kijeshi wa Ujerumani wakati wa vita vya kwanza vya Dunia, Jen. Paul von Hindenburg, Kaiser Wilhelm II, na Jen. Erich Ludendorff.
Viongozi wa kisiasa na kijeshi wa Ujerumani wakati wa vita vya kwanza vya Dunia, Jen. Paul von Hindenburg, Kaiser Wilhelm II, na Jen. Erich Ludendorff.Picha: picture alliance / Everett Collection

Msingi wa uanzishwaji wa Umoja wa Mataifa

Pamoja na hayo, Mwandishi Margaret MacMillan anasema katika kitabu chacke cha Paris 1919: Miezi sita iliyoubadilisha Ulimwengu, kuwa dhana za Baraza la Mataifa zilitumiwa kuchora ramani ya Umoja wa Mataifa.

Miezi michache tu baada ya Ujerumani kusalimu Mei 1945, Marekani ilishinikiza kuundwa kwa Umoja wa Mataifa wakati wa majadiliano mjini San Francisco. Katika historia yake ya miaka 69, umoja huo umekuwa eneo la mijdala mikali, kura za turufu na diplomasia kubwa na utata.

Umoja wa Mataifa pia umekuwa na kasoro zake - vita vya miaka mitatu nchini Syria, na mauaji ya kimbari nchini Rwanda. Mapigano yanaendelea katika Sudan mbili na Somalia, na katika mgogoro mkubwa wa Afrika uliyodumu kwa miaka 15 katika bonde la Congo, licha ya kuweko na idadi kubwa ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Kumekuwepo na utatuzi wa migogoro wenye ufanisi nchini Cambodia, Timor ya Mashariki, Liberia na maeneo mengine, mpaka sasa dunia imefanikiwa kuzuwia uharibifu unaotokana na silaha za nyuklia na mgogoro wa kidunia kwa kiwango cha vita vikuu viwili vya dunia.

Mwandishi wa vitabu Schlesinger anasema Umoja wa Mataifa ni chombo imara zaidi, chenye nguvu kilicho na nafasi ya kudumu muda mrefu kuliko lilivyokuwa Baraza la Mataifa.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae

Mhariri: Mohammed Khelef