1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la mawaziri la Somalia lavunjwa

17 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/Cci6

Waziri mkuu mpya wa Somalia, Nur Hassan Hussein, amelivunja baraza lake la mawaziri wiki mbili tangu lilipoundwa, hivyo kukubali shinikizo la jumuiya ya kimataifa iliyotaka serikali yake iwajumulishe viongozi kutoka sehemu mbalimbali za Somalia.

Bwana Hussein amesema baraza hilo litapunguzwa na kwamba nusu ya mawaziri watateuliwa nje ya bunge. Aidha amesema atawasilisha mapendekezo ya baraza lake la mawaziri bungeni ili yaidhinishwe.

Hussein alilitaja baraza lake la mawaziri lililokuwa na mawaziri 74 mnamo tarehe mbili mwezi huu wa Disemba na kuwateua mawaziri mawili nje ya bunge. Mawaziri watano walijiuzulu siku moja baada ya baraza la mawaziri kutangazwa wakilalamika kwamba hawakushauriwa.

Hussein anategemewa na wengi aiokoe Somalia kutokana na miaka 17 ya maisha magumu na vita vya kimbari vilivyosababisha umwagikaji mkubwa wa damu.

Sambamba na hayo, mwandihsi mmoja wa habari raia wa Ufaransa ametekwa nyara na watu wasiojulikana katika mji wa Bosasso kaskazini mwa Somalia. Watekaji nyara wanataka walipwe dola 70,000 kabla kumuachilia huru.