1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la mpito Sudan yaahidi kuunda serikali ya kiraia

Angela Mdungu
23 Aprili 2019

Msemaji wa Jeshi la Sudan Jenerali Shamseldin Kibashi, amesema, uongozi wa baraza la mpito la kijeshi unafanya mazungumzo na pande zote za kisiasa kupata jina la Waziri mkuu ili kuunda serikali ya kiraia

https://p.dw.com/p/3HGc3
Sudan Militärrat Abdel Fattah al Burhan
Picha: picture-alliance/AA

Kupitia taarifa yake, Jenerali Kibashi ametoa tamko fupi la nia ya kuunda serikali ya kiraia ingawa hakutoa kauli yoyote juu ya matakwa ya waratibu wa maandamano ambao wanataka kuundwa kwa serikali ya kiraia haraka iwezekanavyo. Mvutano umezidi kupambamoto Sudan, baada ya mazungumzo kati ya waandamanaji na baraza la mpito la kijeshi ambalo linaongoza nchi hiyo tangu Rais wa zamani Omar al Bashir alipoondolewa madarakani Aprili 11 mwaka huu kuvunjika.

Waandamanaji hao wanautuhumu uongozi mpya wa kijeshi kwamba una tofauti ndogo kulinganisha na Al Bashir aliyeng'olewa kwenye kiti chake baada ya mandamano yaliyoanza mwezi Desemba mwaka jana. Waratibu wa maandamano hayo wameapa kuyaendeleza maandamano hadi pale matakwa yao yote yatakapo timizwa. Maelfu ya waandamanaji hao walishiriki kwenye maandamano ya Jumatatu katika miji mbali.

Sudan, Khartoum: Sitzblockade vor dem Verteidigungsministerium
Sehemu ya waandamanaji mjini KhartoumPicha: picture-alliance/AA/M. Hjaj

Jeshi lajaribu kupooza msuguano

Hata hivyo Jenerali Kibashi, hapo jana katika kujaribu kuupoza mvutano unaoendelea aliwaambia waandishi wa habari kwamba Baraza la mpito la kijeshi la Sudan linachunguza na kuyafanyia kazi madai ya waandamanaji na kwamba watawasiliana na kila mmoja ili kufikia muafaka.

Naye kiongozi wa Baraza la mpito la kijeshi Jenerali Abdel Fattah Burhani ameahidi kwamba  baraza hilo litawapa madaraka wananchi baada ya makubaliano na pande zote mbili. Jenerali Burhani amesema baraza lake limepokea zaidi ya mitazamo 100 kutoka kwa wadau mbalimbali wa kisiasa nchini humo juu ya hatma ya nchi hiyo yakiwemo mapendekezo kutoka kwa waandamanaji.

Wakati huohuo, Rais wa Misri, Abdel Fatah Al Sisi anakuwa mwenyeji wa mikutano miwili inayoshirikisha viongozi wa nchi za kiafrika huko Sudan na Libya. Baadhi ya Maraisi  wanaohudhuria mikutano hiyo ni kutoka Chad, Djibouti, Somalia na Afrika ya kusini.

Ofisi ya Rais ya Alsisi imeeleza kuwa mikutano hiyo ni ya mashauriano ya nchi washirika wa Sudan ili kujadili maendeleo katika juhudi za kurejesha amani  na utulivu nchini humo. Mkutano wapili una lengo la kujadili maendeleo ya Libya na na namna ya kudhibiti mgogoro, kufufua hali ya kisiasa na kupambana na ugaidi.

Mwandishi: Angela Mdungu/APE/ AFPE

Mhariri: Sekione Kitojo