1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa tamko kuhusu Mali

Admin.WagnerD4 Aprili 2012

Shinikizo la kuwataka wanajeshi walioupindua utawala wa kidemokrasia nchini Mali kuachia madaraka limeongezeka baada ya mataifa yenye nguvu duniani kuzidisha makali ya vikwazo vya kiuchumi dhidi ya wanajeshi hao.

https://p.dw.com/p/14XXd
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: AP

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yo. wanaandaa taarifa ya pamoja kuhusu mzozo huo wa Mali ambapo kura zitapigwa hapo baadae kuhus suala hilo.

Wakati hayo yakiendelea, Ufaransa  nayo imeitisha mkutano wa dharura unaoshirikisha nchi wanachama 15 wa Baraza hilo, kuandaa makubaliano ya tamko la kulaani mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Rais Amadou Toumani Toure hapo Machi 22.

Wajumbe hao pia watajadili kuimarika kwa nguvu za wanamgambo wa Tuareg, wanaopigana bega kwa bega na kundi la Kiislamu la Ansaruddin, ambao hadi sasa wanaendelea kutwaa miji muhimu ya kaskazini mwa nchi hiyo.

Katika kuongeza shinikizo la kurejeshwa utawala wa kidemokrasia nchini humo, mapema leo Marekani nayo imejiunga na Umoja wa Ulaya pamoja na Umoja wa Afrika katika kuwawekea vikwazo vya usafiri wanajeshi hao kwa kuwazuia kuingia katika mipaka yake.

Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani imesema itaendelea kumzuia Kapteni Sanogo na wenziwe hadi hapo watakaporejesha madaraka kwa Rais Toure na kwamba yeyote atakayewaunga mkono wanajeshi hao naye atawekewa vikwazo hivyo.

Licha ya kupewa saa sabini na mbili kutii amri ya kurejesha utawala wa kidemokrasia nchini humo, Kapteni Sanogo amekataa kuachia madaraka ingawa hapo awali aliahidi kurejesha katiba ya nchi hiyo.

Kapteni Amadou Sanogo (kulia) aliyeipindua serikali ya Mali
Kapteni Amadou Sanogo (kulia) aliyeipindua serikali ya MaliPicha: Reuters

Badala yake Kapteni Sanogo ameitisha mkutano wa kitaifa hapo kesho kujadiliana mustakabali wa nchi hiyo, ambayo sasa inaonekana kugawika. Kapteni Sanogo aliwaambia waandishi wa habari kuwa mkutano huo ndio utakaoamua ipi itakuwa hatma bora zaidi kwa nchi hiyo katika masuala ya demokrasia na utawala.

Kwa upande mwengine, wanamgambo wa Tuareg wameedelea na juhudi zao za kutwaa miji muhimu katika nchi hiyo. Vyombo vya habari vya kimataifa vinaarifu kuwa tayari washirika muhimu wa wanamgambo hao katika mapambano ya kudai uhuru wa eneo la Azawad, kundi la Kiislamu la Ansaruddin, wameanza kuamrisha matumizi ya sheria ya Kiislamu kwenye maeneo ambayo wameyachukua kwa kuwakataza wanawake kuvaa suruali.

Vituo vya redio katika mji wa kihistoa wa Timbuktu na miji mengine ya Gao na Kidal vimekatazwa kupiga nyimbo ambazo zinakwenda kinyume na maadili ya Kiislamu.

Tayari vikwazo vilivyowekwa na Jumuiya ya uchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, dhidi ya utawala wa kijeshi wa Mali vimeanza kuyaathri maisha ya watu wa kawaida, kwani huduma muhimu za chakula na mafuta ya petroli zimeanza kuandimika.

Wananchi nchini humo wamekumbwa na hofu kubwa ya kudhoofika kiuchumi na misururu ya watu wanaosubiri mafuta mjini Bamako imanza kushuhudiwa.

Mwandishi: Stumai George/AFPE/APE/

Mhariri: Mohammed Khelef