1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuujadili mzozo wa Ukraine

26 Januari 2015

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linafanya mkutano wa dharura hii leo kujadili mzozo wa mashariki mwa Ukraine baada ya shambulizi la roketi katika mji wa Mariupol kuwaua kiasi ya watu 30 na kuwajeruhi wengine 90

https://p.dw.com/p/1EQNy
Picha: AP

Rais wa Marekani Barack Obama ameahidi kuishinikiza zaidi Urusi baada ya shambulizi hilo lililofanywa siku ya Jumamosi na waasi wanaoungwa mkono na Urusi wanaotaka kujitenga kwa eneo la mashariki mwa Ukraine katika mji wa bandarini wa Maripuol.

Mkutano wa dharura wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa unaotarajiwa kufanyika leo mchana unakuja baada ya nchi wanachama 15 wa baraza hilo kushindwa kukubaliana siku ya Jumamosi kufikia azimio la kulaani shambulizi hilo baada ya Urusi kupinga juhudi hizo.

Baraza hilo limekutana takriban mara 30 tangu mzozo wa Ukraine kuanza lakini limeshindwa kutoa maamuzi muhimu kutokana na baadhi ya nchi wanachama wa kudumu kama Urusi kutumia kura yao ya turufu kupinga kupitishwa kwa maazimio.

Ukraine yasema ina thibitisho Urusi inahusika

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko amesema katika mkutano wa dharura wa kiusalama kuwa nchi yake imenasa mawasiliano ya simu yanayothibitisha kuwa shambulizi hilo lilifanywa na magaidi wanaopokea usaidizi kutoka Urusi.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko
Rais wa Ukraine Petro PoroshenkoPicha: picture-alliance/dpa/M.Lazarenko

Obama amesema ataangalia ni njia zipi atakazotumia sasa kumzuia mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kuendeleza vita ambavyo vinalenga kuidhoofisha sekta ya kiviwanda ya Ukraine.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa upande wake alimpigia simu Rais Putin hapo jana kumhimiza kuwashinikiza waasi hao wa mashariki mwa Ukraine kusitisha mashambulizi ambayo yameitia wasiwasi mkubwa jumuiya ya kimataifa.

Msemaji wa Merkel, Steffen Seibert amesema Kansela huyo amemtaka Putin kutumia ushawishi wake kuwazuia waasi kutanua uasi wao baada ya mashambulizi ya Mariupol yaliyowaua watu thelathini.

Waasi watakiwa kurejea kwa mazungumzo

Merkel pia amewataka viongozi wa waasi hao kurejea katika meza ya mazungumzo baada ya kujiondoa kutoka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa Minsk mnamo mwezi Septemba mwaka jana na pia ametuma risala za rambi rambi kwa Rais wa Ukraine Poroshenko kufuatia mauaji hayo ya Mariupol.

Maafa baada ya shambulizi mjini Mariopul,mashariki mwa Ukraine
Maafa baada ya shambulizi mjini Mariopul,mashariki mwa UkrainePicha: picture-alliance/dpa/D.Bodrov/TASS

Rais wa halmashauri kuu ya umoja wa Ulaya Donald Tusk ameyataja mashambulizi hayo kama thibitisho kuwa kumfurahisha mchokozi ni kumhimiza kufanya vitendo vikubwa vya mashambulizi na Rais wa Ufaransa Francois Hollande ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusiana na mashambulizi hayo alipofanya mazungumzo na Tusk na Poroshenko.

Urusi imekanusha kuhusika katika kuwapa silaha na ufadhili waasi wa mashariki mwa Ukraine. Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amelilaumu jeshi la Ukraine kwa kuuchochea mzozo kutokana na kufanya mashambulizi kila mara ambayo yamekikua makubaliano ya Minsk.

Rais Poroshenko ameutaka Umoja wa Ulaya kuiwekea Urusi vikwazo zaidi na kuongeza serikali yake inasalia kuunga mkono kupatikana kwa suluhu ya amani. Mawaziri wa mambo ya nje wa umoja huo wanafanya kikao maalum Alhamisi wiki hii kuujadili mzozo huo wa Ukraine.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/Ap

Mhariri:Josephat Charo