1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yataka mapigano kusitishwa Libya

Amina Mjahid Gakuba Daniel
13 Septemba 2019

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limerejelea tena wito wake kutaka usitishwaji wa mapigano Libya, huku likisema hapatakuwa na suluhisho la kijeshi katika mapigano yaliyoanzishwa na mbabe wa kivita Khalifa Haftar

https://p.dw.com/p/3PXD2
UN Sicherheitsrat Beschluss Entsendung ziviler Beobachter in den Jemen
Picha: Reuters/C. Allegri

Katika azimio la pamoja baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa limeongeza muda wa ujumbe wake wa kisiasa nchini Libya hadi septemba 15 mwaka 2020, huku likitaka mataifa yaliyo na ushawishi kwa vyama vya kisiasa nchini humo, kutumia nafasi hiyo kuhimiza usitishaji wa mapigano na kuanza tena mchakato wa kutafuta suluhu ya kisasa utakaosimamiwa na Umoja huo.

Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya mwaka 2011 yalimuondoa madarakani  rais wa muda mrefu nchini humo Muammar Gadhafi ambaye pia aliuawa. Katika vurugu zilizofuatia baadae ziliifanya nchi hiyo kugawika na kuwa na serikali mbili, moja inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa mjini Tripoli na nyengine inayoendeshwa na mbabe wa kivita Khalifa Haftar

Haftar alianzisha mashambulio ya kushtukiza ya kijeshi mnamo Aprili 4 yaliyolenga kuudhibiti mji mkuu Tripoli, licha ya kuonesha dhamira ya wazi ya kuhudhuria mkutano wa kitaifa wiki kadhaa baadae uliyonuiwa kuundwa serikali ya pamoja ili kufungua njia ya kufanyika uchaguzi katika taifa hilo tajiri kwa mafuta la Kaskazini mwa Afrika.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lasema linahofu ya uadui unaoendelea libya

Italien 2018 | Chalifa Haftar, Warlord Libyen
Mbabe wa kivita nchini Libya Khalifa Haftar Picha: Getty Images/AFP/F. Monteforte

Jeshi lake limejipanga vizuri likilinganishwa na majeshi mengine ya waasi. Khalifa Haftar anaungwa mkono na mataifa kama Misri, Umoja wa falme  za kirabu na Urusi. Jeshi lake  limekumbana na mapambano makali kutoka kwa wapiganaji wanaojifungamanisha na serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa inayoungwa mkono pia na Uturuki na Qatar.

Baraza hilo la Usalma la Umoja wa Mataifa limeelezea wasiwasi wake juu ya uadui unaoendelea ndani na maeneo ya mji wa Tripoli na hatua ya kulengwa kwa majengo ya raia katika mapigano hayo, pamoja na kupanuliwa kwa mgogoro huo zaidi na magaidi pamoja na makundi yaliyo na itikadi kali na pia kudorora kwa  hali mbaya ya kibinaadamu.

Kulingana na Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Libya Ghassan Salame,  tangu mwezi Aprili  zaidi ya raia 100 wameuwawa na wengine 300 kujeruhiwa. Aidha, watu wengine 120,000 wamekosa makaazi. Mjumbe huyo amesema hadi sasa idadi kamili ya wapiganaji waliouwawa katika vurugu hizo haijulikani lakini inakadiriwa kuwa chini ya wapiganaji 1000.

Chanzo: ap/afp