1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama laijadili Syria

20 Machi 2012

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaanza kujadili rasimu ya tamko la mataifa ya Magharibi juu ya Syria lililowasilishwa na Ufaransa huku Urusi ikitaka usitishwaji wa mapigano wa muda kuruhusu msaada wa kibinaadamu.

https://p.dw.com/p/14NgC
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likijadili taarifa kuhusu Syria.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likijadili taarifa kuhusu Syria.Picha: dapd

Sasa Urusi nayo imepaza sauti yake kuhusiana na maafa ya kibinaadamu katika maeneo yanayokabiliwa na mapigano nchini Syria. Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi hiyo, Sergei Lavrov, amekutana na mkuu wa Shirika la Msaada Mwekundu, Jakob Kellenberger, na kwa pamoja viongozi hao wameitaka serikali ya Rais Assad kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na upinzani, ili kuruhusu mashirika ya misaada kuwafikia watu walioathirika.

Katika kauli nyengine inayoweza kuwa ya kwanza kutolewa na uongozi wa juu wa Urusi kuhusu Syria, Lavrov amesema nchi yake haikubaliani na mambo kadhaa yanayofanywa na serikali ya Syria na kwamba inachotaka ni kuanza kwa mazungumzo ya amani.

"Hatuiungi mkono serikali ya Syria. Tunaunga mkono kuanza kwa mchakato wa kisiasa. Na ili hilo lifanikiwe, ni muhimu kusitisha mapigano. Tutafanya kila kinachowezekana, licha ya maamuzi yanayofanywa na serikali ya Syria, ambayo mengi yao bila ya shaka hatukubaliani nayo." Amesema Lavrov.

Urusi yataka Msalaba Mwekundu waruhusiwe

Urusi pia imeitaka serikali ya Assad kuliruhusu Shirika la Msalaba Mwekundu kuwatembelea mahabusu wote wa kisiasa. Marekani imekaribisha kile ilichokiita "kubadilika kwa mtazamo wa Urusi juu ya Syria," ambapo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Victoria Nuland, amewaambia waandishi wa habari kuwa kauli hiyo ya Urusi ni "hatua nzuri".

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, sergei Lavrov (kulia) akizungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataita, Ban Ki-moon kuhusiana na Syria.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, sergei Lavrov (kulia) akizungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataita, Ban Ki-moon kuhusiana na Syria.Picha: dapd

Kauli hii ya Urusi inafungua njia kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambako hivi leo yanafanyika mazungumzo ya kwanza kuhusiana na rasimu ya tamko la mataifa ya Magharibi juu Syria.

Pamoja na kuunga mkono jitihada za mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwa Syria, Koffi Annan, tamko hilo linazungumzia uwezekano wa kuchukuliwa "hatua zaidi" dhidi ya Rais Assad, endapo ndani ya siku saba baada ya kupitishwa kwake, kiongozi huyo hatakubaliana kikamilifu na mpango wa amani wenye vipengele sita, uliopendekezwa na Annan.

Ufaransa yataka hatua za haraka

Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Gerard Araud, amesema anatarajia kuwa tamko hilo litajadiliwa, kupitishwa na kuanza kutekelezwa leo. Nakala ya tamko hilo iliyopatikana na shirika la habari la AFP, inazungumzia wasiwasi mkubwa juu ya kuzorota kwa hali nchini Syria na masikitiko makubwa kwa maelfu ya watu waliopoteza maisha katika kipindi cha mwaka mmoja tangu maandamano ya umma dhidi ya utawala yaanze.

Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa, Gerard Araud.
Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa, Gerard Araud.Picha: AP

Mara mbili tafauti, Urusi na China zimetumia kura zao za turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya maazimio juu ya Syria. Nchi hizo zilisema kwamba maazimio hayo yalikuwa yanakusudia kuondosha utawala na kwamba zilikuwa zinapinga vikwazo vyovyote vile.

Kwa sasa, Baraza la Usalama linajadili taarifa kwa vyombo vya habari ambayo imependekezwa na Urusi kulaani mashambulizi ya mabomu ya mwishoni mwa wiki kwenye miji ya Allepo na Damascus. Mapigano ya jana kati ya vikosi vya serikali na vya upinzani mjini Damascus yalisababisha vifo vya watu watatu.

Mashambulizi na mapigano haya ya karibuni katika ngome kuu za utawala wa Assad, yametajwa kuwa dalili nyengine inayoonesha kuwa Syria imo katika hatua za awali za vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba