1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la usalama lakataa ombi la Urusi kuhusu Kosovo

18 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D9CZ

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limekataa ombi la Urusi kulitaka liutangaze uhuru wa Kosovo kuwa usio halali.

Balozi wa Urusi katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin, amesema hatua ya Kosovo kujitangazia uhuru kutoka kwa Serbia inakiuka azimio la mwaka wa 1999 la umoja huo kuhusu Kosovo.

Hata hivyo, kufuatia mkutano wa dharura wa baraza la usalama uliofanyika faraghani, balozi wa Uingereza katika umoja wa Mataifa, John Sawers, amewaambia waandishi wa habari kwamba hakuna hata nchi moja kati ya nchi 14 wanachama wa baraza hilo inayounga mkono msimamo wa Urusi.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana leo kujadili zaidi swala la Kosovo.

Pia mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kukutana hii leo mjini Brussels Ubelgiji kujadili taarifa ya pamoja ya umoja huo kuhusu hatua ya Kosovo kujitangazia uhuru wake kutoka kwa Serbia.