1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la usalama laonya kuhusu vita Cote d'Iovire

4 Machi 2011

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeonya juu ya kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Cote d'Ivoire na limewataka wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja huo nchini humo watumie kila njia kuwalinda raia

https://p.dw.com/p/10TL2
Alain Le Roy, mkuu wa juhudi za kulinda amaniPicha: AP

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali ya usalama inayoendelea kuzorota nchini Cote d'Ivoire na kuwataka wanajeshi wa tume ya kulinda amani ya umoja huo wachukue hatua zaidi kuwalinda raia.

Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na juhudi za kulinda amani, Alain Le Roy, ameliambia baraza la usalama kwamba vikosi vya usalama vya rais wa Cote d'Ivoire Laurent Gbagbo, hapo jana vilitumia silaha nzito dhidi ya waandamanaji wanawake na kuwaua wasiopungua wanane. Wanawake hao waliokuwa wakiandamana kumtaka rais Gbagbo ajiuzulu na akabidhi madaraka kwa Alassane Ouattara, anayetambulika na jamii ya kimatafia kama mshindi wa uchaguzi wa rais wa Novemba 28 mwaka jana.

Mauaji yalaaniwa

Baraza la usalama limeyalaani vikali mauaji hayo pamoja na vitisho na machafuko yanayofanywa na vikosi vya Gbagbo dhidi ya raia na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa.

Balozi wa Cote d'Ivoire katika Umoja wa Mataifa, Youssoufou Bamba, amesema, "Wanawaua watu kwa misingi ya kikabila. Wanawaua raia wa nchi za kigeni, nchi jirani. Hiyo haikubaliki. Leo katika karne hii ya 21 ambapo watu wanachukua jukumu na kudai demokrasia na uhuru zaid, mauaji hayo hayakubaliki."

Youssoufou Bamba UNO Elfenbeinküste
Youssoufou Bamba, balozi wa Cote d'Ivoire katika Umoja wa MataifaPicha: picture alliance/dpa

Wizara ya mambo ya ndani ya Marekani imesema mauaji ya wanawake hao yanaashiria ukosefu wa maadili wa rais Gbagbo.

Tume ya amani yatakiwa kuwalinda raia

Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa, ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa baraza la usalama, Li Baodong, amesema wamejadili mauaji hayo na kuitaka tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa nchini Cote d'Ivoire itumie uwezo wake wote kutekeleza wajibu wake, hususan kuwalinda raia.

Umoja wa Mataifa unasema watu 50 wameuwawa katika kipindi cha wiki moja iliyopita. Msemaji wa umoja huo anayehusika na masuala ya haki za binadamu nchini Cote d'Ivoire, Guillaume Nguefa, amesema watu takriban 26 wameuwawa katika kitongoji cha Abobo katika kipindi cha saa 24 zilizopita. Watu zaidi ya 200,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao katika kitongoji hicho, tangu mapigano yalipozuka wiki iliyopita.

Baraza la usalama limezitaka pande husika ziwe na uvumilivu na zijiepushe na machafuko na kumtaka rais Gbagbo aache kuizingira hoteli ya Golf mjini Abidjan, ambayo ni makao makuu ya tume ya Umoja wa Mataifa.

Gbagbo anakataa kuondoka madarakani licha ya kushindwa na Alassane Ouattara katika uchaguzi wa Novemba 28 mwaka jana, na anautaka Umoja wa Mataifa uondoke Cote d'Ivoire.

Marais watano wa Afrika walioteuliwa na Umoja wa Afrika kuutafutia ufumbuzi mzozo wa nchi hiyo, wanakutana leo nchini Mauritania na huenda baadaye wakaelekea Abidjan kuwasilisha matokeo ya mashauriano yao kwa viongozi wanaohasimiana.

Uchunguzi wa silaha

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa unachunguza silaha zinazoshukiwa kusafirishwa Cote d'Ivoire kutoka Zimbabwe, kinyume na vikwazo vya umoja huo. Kwa mujibu wa ripoti ya usimamizi wa vikwazo ya mwezi Januari mwaka huu, iliyopatikana na shirika la habari la Reuters, tume ya amani ya umoja wa mataifa nchini Cote d'Ivoire inachunguza shehena ya masunduku 10 makubwa ya mbao ambayo huenda yana magari na vifaru. Shehena hiyo imekuwa katika bandari ya Abidjan kwa miezi sita.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/AFPE/APE

Mhariri: Hamidou Oummilkheir