1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barosso ataka uratibu wa uchumi kuimarishwa

6 Januari 2011

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya José Manuel Barroso ametoa mwito wa kuwepo uratibu zaidi katika sera za kiuchumi ndani ya umoja huo

https://p.dw.com/p/zuE0
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya José Manuel Barroso na Kansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: AP

Alipogusia mzozo unaohusika na sheria mpya ya Hungary kuhusu vyombo vya habari,Barroso alikumbusha kuwa uhuru wa vyombo vya habari ni msingi unaothaminiwa na kuheshimiwa katika Umoja wa Ulaya.

Kwa maoni ya Halmashauri ya Umoja wa Ulaya,kwa sasa hakuna hatari kubwa ya kuvurugika kwa utulivu katika eneo la sarafu ya Euro.

Euro i salama!

Kwa hivyo huu ndio wakati wa kushughulikia mipango ya muda mrefu, kwani imedhihirika kuwa tofauti kubwa za kiuchumi kati ya nchi wanachama ni hali iliyozusha mzozo wa Euro.Muungano wa sarafu, hauwezi kufanya kazi bila ya kuwepo uratibu zaidi, katika sera za kiuchumi.

Na hayo si maoni ya halmashauri hiyo tu, kwani nchi wanachama wengi pia zinaamini hivyo. Juu ya hivyo, upinzani ni mkubwa sana dhidi ya kile kilichoitwa na wengi wao "serikali ya uchumi". Lakini hakuna njia nyingine, "Sio tu wanaoamini mfumo huo, ndio wanaotaka uongozi na ushirikiano zaidi wa kiuchumi. Hata masoko na washirika wetu wa kimataifa pia wanatazamia hilo," anaonya Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya José Manuel Barroso

Flash-Galerie Ungarn EU-Präsidentschaft Protest gegen Mediengesetze
Magazeti ya Hungary yaliyochapisha kurasa tupu:Sheria mpya inaaminika kuvibana vyombo vya habariPicha: AP


Nishati na Ushirikiano

Barroso anataka ushirikiano zaidi katika sekta ya nishati vile vile. Kwa maoni yake,huo utakuwa mradi mpya wa kujijumuisha. Kwa hivyo, viongozi wa taifa na serikali wa Umoja wa Ulaya, watakapokutana mwanzoni mwa mwezi wa Februari, mkutano huo unataka kushughulikia zaidi,mada ya nishati.Anasema, bado kunakosekana soko la nishati linalofanya kazi katika kanda hiyo.

Katika mkutano wake na waandishi habari mjini Brussels siku ya Jumatano, Barroso hakuweza kuepukana na mada ya utata. Hiyo inahusika na sheria mpya ya vyombo vya habari nchini Hungary,inayoshika wadhifa wa urais wa kupokezana katika Umoja wa Ulaya. Wakosoaji wanasema, serikali ya Hungary inajaribu kuvibana vyombo vya habari vinavyokosoa. Kwa maoni ya Barroso sasa ni mapema mno kuamua kuhusu sheria hiyo mpya.

No Flash Verbraucherpreise Eurozone Euro Preise
Noti na sarafu za euro:Hofu ya kutikisika ipoPicha: AP

Hata hivyo alisema wazi wazi kuwa,"Tumeeleza baadhi ya hofu zetu. Bila shaka, tungependa kupata ufafanuzi kutoka kwa serikali ya Hungary na ikiwezekana kuondosha hofu hizo. Lakini moja lifahamike, uhuru wa vyombo vya habari ni msingi unaoheshimiwa katika Umoja wa Ulaya." alifafanua.

Barroso ameahidi kuzungumzia mada hiyo atakapokutana na Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban wakati wa ziara yake ya hii leo mjini Budapest.

Mwandishi: Hasselbach,Christoph/ZPR

Mpitiaji:Charo,Josephat