1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bashar al-Assad hastahili katika mustakabali wa Syria

11 Aprili 2017

Rais Bashar al-Assad hastahili kuwa katika mustakabali wa nchi ya Syria, ndiyo kauli iliyotolewa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson.

https://p.dw.com/p/2b4sM
Belgien Rex Tillerson in Brüssel
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Rex TillersonPicha: DW/B. Riegert

Tillerson aliyasema haya wakati ambapo mataifa saba yaliyoendelea zaidi kiviwanda duniani yanayounda kundi la G7 yalipokamilisha mkutano wao huko Lucca, Italia, Jumanne na kukataa kuziwekea vikwazo vipya Urusi na Syria.

Wakati ambapo Mawaziri hao wa G7 walikuwa wakishinikiza kumalizwa kidiplomasia kwa mzozo wa miaka sita na kubuniwa kwa taifa lenye amani ya kudumu la Syria, Tillerson amesema matumaini yao ni kwamba Bashar al-Assad hayuko katika mpango huo walio nao juu ya nchi hiyo.

Tillerson amesema anataraji kwamba serikali ya Urusi itafahamu kwamba imefanya urafiki na mtu asiyeeleweka Bashar al-Assad, kwani nchi zote mbili zilitia saini mkataba wa kutotumia zana za kemikali na kwa sasa, Assad ameigeuka Urusi.

Pengo kati ya Marekani na Urusi laongezeka

"Nadhani ni muhimu kufikiria suala kwamba Urusi imefanya usuhuba na uongozi wa Assad, Wairan na Hezbollah," alisema Tillerson, "je huo ni muungano wa muda mrefu unaokidhi mahitaji ya Urusi? au Urusi ingependelea kuwa katika muungano na Marekani, na nchi nyengine za Magharibi na Mashariki ya Kati zilizo na nia ya kuumaliza mzozo wa Syria? Tunataka kumaliza mateso wanayopitia Wasyria," aliongeza waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani.

Syiren Präsident Bashar al-Assad Interview
Viongozi wa G7 wanataka Urusi isitishe usuhuba na Bashar al-AssadPicha: Reuters

Huku pengo likiendelea kuongezeka kati ya Marekani na mwandani wa Assad, Urusi, mawaziri hao wa G7 wameonesha kumuunga mkono Tillerson aliewasili mjini Moscow kipindi kifupi baada ya kukamilika mkutano wa G7, Italia, kwa mazungumzo muhimu na waziri mwenzi wake Sergei Lavrov.

Sigmar Gabriel ni waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani aliyehudhuria mkutano huo wa G7 na alisema, "Kivyangu nimefurahia sana jinsi waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson alivyochukua msimamo wa wazi hapa," alisema waziri huyo, "tunamuunga mkono kikamilifu katika juhudi zake mjini Moscow, ili awapelekee Warusi kufuata mwelekeo huu wa kisiasa na wauunge mkono ili vita visitishwe." 

Ziara ya Tillerson Moscow itaonesha iwapo Marekani inataka kuumaliza mzozo Syria

Kauli ya waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson kwamba kuwekwe vikwazo vipya dhidi ya Urusi ili isitishe kuiunga mkono serikali ya Assad haikukubaliwa, kwani baadhi ya mawaziri hao wamekubaliana kwamba njia ya majadiliano ndiyo inayostahili kufuatwa katika suala hilo.

USA UN Sicherheitsrat - Boris Johnson
Waziri wa masuala ya nje wa Uingereza Boris JohnsonPicha: picture alliance/Photoshot

Lakini Johnson amesema huenda bado kukawekwa vikwazo kwa wanajeshi wa Urusi iwapo uchunguzi huru wa shambulizi la kemikali utawahusisha, na wakati huo huo akaongeza kuwa Urusi inastahili kujiondoa kwenye mzozo huo wa Syria.

"Bila shaka kila mmoja anafahamu kwamba Urusi ina malengo ya kisiasa na ya kibinafsi nchini Syria," alisema Johnson, "hayo yote yanaweza kuheshimiwa ila wakati huo huo Urusi inahitaji kuondoka kwenye balaa hili la Syria. Lazima mtu agharamie ujenzi mpya wa Syria na haitokuwa Urusi," aliongeza Johnson.

Hayo yakiarifiwa ziara ya Rex Tillerson mjini Moscow itaonesha iwapo uongozi wa Donald Trump unaweza kupanga na kumaliza vita vya Syria, kwa kuendeleza mori uliotokana na shambulizi lake wiki jana. Urusi ilisema Jumatatu kwamba Tillerson hajapangiwa kukutana na rais Vladimir Putin hatua ambayo huenda ikazusha taharuki.

Mazungumzo hayo yatapima uwezo wa Tillerson wa majadiliano ya kidiplomasia kwani wasifu wake unaonesha hana uzoefu huo.

Mwandishi: Jacob Safari/AP/AFP/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga