1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayer yainunua Monsanto

Sekione Kitojo
7 Juni 2018

Kampuni kubwa la Ujerumani linalotengeneza madawa na kemikali la Bayer limesema  miaka miwili ya kufuatilia ununuzi wa kampuni  ya Monsanto imefika mwisho, na makampuni hayo yalitia saini makubaliano ya kuungana.

https://p.dw.com/p/2z66X
Bayer AG Logo
Picha: picture-alliance/Geisler/C. Hardt

Makampuni  hayo  sasa  yameunda  kampuni  kubwa  kabisa  la  madawa  ya  kilimo  likiwa  na dhamira  kubwa  ya  kuilisha  dunia lakini  wakati  huo  huo ikishambuliwa  na wanaharakati  wanaotetea mazingira.

EU Bayer Monsanto - Margrethe Vestager
Kamishna wa ushindani wa Umoja wa Ulaya margrethe Vestager akizungumza na waandishi habari kuhusu muungano wa Bayer na MonsantoPicha: Reuters/F. Lenoir

"Kulisha idadi  ya  watu  inayoongezeka  duniani  ni  lengo  lake  la muda  mrefu, na  tunataka  kuchangia  katika  utatuzi wa  suala  hilo," mtendaji  mkuu  wa  kampuni  ya  Bayer  Werner Baumann aliliambia gazeti  la  masuala  ya  biashara  la  Handelsblatt  katika  mahojiano siku  ya  Jumanne. Watendaji  wanatabiri  mambo  makubwa  katika makadirio  kwamba  kiasi  ya  watu  bilioni  10  watakuwa  wanaishi katika  dunia  hii ifikapo  mwaka  2050, ikiwa  na  maana  ya kwamba  chakula  kingi  zaidi  kinalazimika  kulimwa  katika  eneo  lile lile  la  ardhi inayoweza  kulimwa.

Wanasema  hilo  linawezekana  kufanikishwa  kwa  njia  bora  zaidi kwa kutumia  teknolojia  zinazopuuzwa  na  mashirika  ya  ulinzi  wa mazingira  pamoja  na  wanasiasa, ikiwa  ni pamoja  na  mbegu zilizobadilishwa  vinasaba ambazo zimetayarishwa  kwa  kupambana na  madawa  makali  ya  kuuwa  wadudu.

9885 Die Saat der Gier – Wie Bayer mit Monsanto die Landwirtschaft verändern will
Bayer na Monsanto ni kampuni linalotaka kufanya mageuzi katika kilimoPicha: Autentic

Mimea  iliyobadilishwa  vinasaba  pamoja  na  vifaa  vya  digitali kuwasaidia  wakulima  waweze  kujiweka  katika  hali  ya kupambana  na  hali  ya  hewa  na  kuangalia  afya  ya  mashamba yao  kunaweza  pia  kusaidia  kuongeza  mazao  ambayo yanatishiwa  na  mabadiliko  ya  tabia  nchi.

Malengo endelevu

"Tutawasaidia  wateja  wetu  kulima  mazao  mengi  zaidi kwa gharama  nafuu,"  Baumann  aliwaambia  waandishi  habari  siku  ya Jumatatu, wakati  huo  huo  akiahidi  kwamba  " tutaweka  msukumo huo  huo  katika  kufanikisha  malengo  yetu endelevu kama tunavyofanya  katika  malengo  yetu  ya  kifedha."

"Suala  muhimu  litakuwa  iwapo Bayer  ni  imara  vya  kutosha kujitenganisha," gazeti  la  Handelsblatt  limetabiri.

"Kwa  upande  mmoja  ni  wa  biashara  ambapo  ni  muhimu  kupata fedha  nyingi  za  kutosha  kwa  ulinzi wa  mimea  kupitia  madawa na  mbegu  kama  wanavyotaka  wawekezaji. Kwa  upande mwingine , Bayer  inahitaji  kupata  kuaminika  na  umma  ambao unaendelea  kuwa  shaka  shaka  juu  ya  kilimo kinachoongozwa  na viwanda.

Bonn Bayer Hauptversammlung CEO Werner Baumann
Mwenyekiti mtendaji wa Bayer Werner BaumannPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Meissner

Kufuatia  kuungana  kwa  Dow na  DuPont mwaka  2017  na ChemChina  kununua  kampuni  la  Uswisi  la  Syngenta ,  kujapamoja kwa  Bayer  na  Monsanto  ni  muungano  mkubwa  kabisa  katika wimbi  la  makampuni  makubwa  kuungana  katika  viwanda  vya kemikali ambayo  yameunda  muungano  mkubwa  kabisa  katika bara   la  Ulaya, Marekani  na  Asia.

Tangu ilipozinduliwa  mwaka  2016, ndoa  hii  ya  Bayer na Monsanto  itaunda  kundi  kubwa  kabisa  la  makampuni  likiwa  na wafanyakazi  115,000 na  mapato  ya  kila  mwaka  ya  euro  bilioni 45.

Bonn Anti Bayer Monsanto Protest
Wapinzani wa muungano wa Bayer na Monsanto wakionesha kutoridhishwa kwao na shughuli za makampuni hayo.Picha: Reuters/W. Rattay

Maafisa  wanaoangalia  ushindani  waliilazimisha  Bayer  kuuza sehemu  ya  biashara  yake  ya  hivi  sasa  ya  mbegu na  madawa ya   kilimo, ambayo  yalikuwa  yanaiingizia  kampuni  hiyo  kiasi  cha euro  bilioni  2.2 kwa  mwaka , kwa  kampuni  washindani  wake  la BASF  kabla  ya  kuruhusu makubaliano  hayo.

Bayer  ina nia ya  kupunguza  mbinyo  kutoka  kwa  walinzi  wa mazingira  na  wanasiasa  kama  ilivyo kwa  wawekezaji  pia. Upinzani  duniani  kote  dhidi  ya  kilimo  kinachoendeshwa na viwanda  na  hususan Monsanto  umesababisha  watendaji kutangaza  wiki  hii  kwamba  jina  hilo  linaachwa.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Iddi Ssessanga