1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern katika fainali ya Ligi ya Mabingwa

26 Aprili 2012

Bayern Munich wamefuzu katika fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya jana usiku baada ya kushinda mikwaju ya penalti 3 - 1 dhidi ya Real Madrid uwanjani Santiago Bernabeu Uhispania.

https://p.dw.com/p/14l5S
Bayern Munich's players celebrate victory against Real Madrid after their Champions League semi-final second leg soccer match at Santiago Bernabeu stadium in Madrid, April 25, 2012. REUTERS/Felix Ordonez (SPAIN - Tags: SPORT SOCCER)
Champions League Halbfinale Real Madrid FC Bayern MünchenPicha: Reuters

Mikwaju hiyo ya penalti ilipigwa baada ya Real kushinda pambano hilo la mkondo kwa pili magoli mawili kwa moja, ambao uliyafanya matokeo jumla ya magoli matatu kwa matatu kwa sababu Bayern walikuwa wameshinda mkondo wa kwanza magoli mawili kwa moja.

Bastian Schweinsteiger aliifungia Bayern penalti ya ushindi, baada ya kipa Manuel Neuer kuiokoa mikwaju ya nyota wa Real Cristiano Ronaldo na Kaka. Katika fainali, ambayo itachezewa uwanja wao wa nyumbani Allianz Arena, mjini Munich, Bayern watakutana na Chelsea, ambao waliwashinda Barcelona Jumanne usiku kwa jumla ya magoli matatu kwa mawili. Bayern itakuwa timu ya kwanza kucheza fainali ya ligi ya mabingwa katika uga wao wa nyumbani tangu AS Roma, ambao walishindwa na Liverpool kupitia mikwaju ya penalty katika mwaka wa 1984.

Mourinho: Real walikuwa na uchovu
Kocha wa Real Jose Mourinho ambaye pia alishindwa kupitia penalti katika mechi ya nusu fainali alipokuwa kocha wa Chelsea mnamo mwaka wa 2005, dhidi ya Liverpool, aliwapongeza vijana wake ijapokuwa alisema walikuwa na uchovu kutokana na mchuano wa mwisho wa wiki iliyopita ambapo waliwashinda barca. Alisema walikuwa na kazi ngumu wakati Bayern nao walikuwa wamepumzika vya kutosha.

Real Madrid walikuwa miamba ya pili Uhispania kuanguka katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa
Real Madrid walikuwa miamba ya pili Uhispania kuanguka katika nusu fainali ya Ligi ya MabingwaPicha: Reuters

Mourinho alikataa kumshutumu Ronaldo kwa kushindwa kufunga mkwaju wake, akisema kitu kama hicho kilitokea jana usiku kwa nyota wa Barca Lionel Messi, lakini wote ni wachezaji wazuri. Alisema hayo ndiyo yanayotokea katika kandanda wakati mwingine, akiongeza kuwa anawahurumia zaidi wachezaji kuliko yeye mwenyewe.

Lakini hata baada ya kushindwa jana, mkufunzi wa Real Madrid Jose Mourinho ameahidi kusalia katika klabu hiyo. Alisema ikiwa wachezaji pamoja na klabu wanamtaka aendelee na kazi basi atafanya hivyo. Mourinho ana mkataba na klabu hiyo hadi mwaka wa 2014. Mlinda lango wa Real Iker Casillas alimudu kuokoa mikwaju miwili ya penalty za Bayern.

Timu zote zilifanya mashambulizi
Ronaldo aliwapa Real uongozi katika dakika ya sita kupitia penalty baada ya beki chipukizi wa kushoto kwa upande wa Bayern, David Alaba alipounawa mpira kutokana na kombora lililopigwa na Angel Di Maria. Ronaldo kisha alifunga bao safi katika dakika ya 15 baada ya kupokea pasi maridadi kutoka kwake Mezut Ozil, na kufanya mambo kuwa mbili kwa sifuri.

Katika dakika ya 28, Bayern walipewa penalty baada ya mchezaji Pepe kumsukuma Mario Gomez katika eneo la hatari. Iker Casillas alimudu kuufikia mpira lakini kombora la Robben likaingia nyavuni na kufanya mambo kuwa mbili kwa moja. Hivyo basi baada ya dakika 90 za mchezo, ilibidi kuongezwa dakika 30 za ziada ambacho kiliisha sare ya bila kufungana na hivyo mikwaju ya penalty ikaamua mshindi.

Kipa wa Bayern Manuel Neuer alikuwa shujaa Santiago Bernabeu
Kipa wa Bayern Manuel Neuer alikuwa shujaa Santiago BernabeuPicha: Reuters

Kocha wa Bayern Jupp Heynckes aliusifu mchezo huo ambao ulichezewa uwanja aliowahi kuhudumu kama kocha. Heynckes alishinda kombe la Mabingwa katika msimu wake wa pekee wa 1997-98 akiwa na klabu hiyo ya Real Madrid. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 66 aliwapongeza wachezaji wake pamoja wote wanaofanya kazi katika klabu hiyo.

Pamoja na uwezekano wa kutwaa kombe hilo la mabingwa, Bayern pia wana nafasi ya kushinda kombe la Shirikisho watakapokutana na mabingwa wapya wa ligi ya soka ya ujerumani Bundesliga Borussia Dortmund katika fainali mnamo tarehe 12 Mei mjini Berlin, wiki moja kabla ya kuwaalika Chelsea.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Mohamed Khelef