1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern mguu mmoja katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa

29 Machi 2012

Miamba ya Bundesliga Bayern Munich waliiweka hai ndoto ya kucheza fainali ya ligi ya Mabingwa katika mji wao wa nyumbani. Hii ni baada ya kushinda mchuano wa mkondo wa kwanza wa robo fainali dhidi ya Olympique Marseille

https://p.dw.com/p/14U9j
Mario Gomez (L) of Bayern Munich celebrates with team mate after scoring against Olympique Marseille during their Champions League quarter-final first leg soccer match at Velodrome Stadium in Marseille March 28, 2012. REUTERS/Robert Pratta (FRANCE - Tags: SPORT SOCCER)
Champions League 2011 / 2012 Viertelfinale Olympique Marseille gegen FC Bayern München HinspielPicha: Reuters

Magoli katika kila kipindi kutoka kwa Mario Gomez na Arjen Robben yaliipa Bayern Munich ushindi wa mabao mawili kwa sifuri nyumbani kwa Olympique Marseille Jana Jumatano. Ushindi huo umewaweka miamba hao wa ligi ya soka Ujerumani – Bundesliga hatua moja karibu na nusu fainali ya kombe la Mabingwa barani Ulaya maarufu kama UEFA Champions League.

Wakati huo huo, mabingwa wa ulaya Barcelona walitoka sare ya bila kufungana na viongozi wa ligi ya soka Italia Serie A AC Milan uwanjani San Siro na kuwacha nafasi ya robo fainali kusalia wazi.

Ushindi wa Bayern unawafanya kuwa timu bora inayopigiwa upatu kufuzu kwa nusu fainali dhidi ya Real Madrid ambao siku ya Jumanne walishinda magoli matatu wka sifuri nyumbani kwa APOEL Nicosia katika mechi y amkondo wa kwanza.

Bayern iliumiliki mpira

Mshambuliaji wa Bayern Mario Gomez alifunga bao lake la 11 la ligi ya Mabingwa msimu huu ikiwa imesalia dakika moja kipindi cha kwanza kukamilika katika uga wa Stade Veledrome, alipoichukua pasi kutoka wka mwenzake Arjen Robben na kusukuma kombora ambalo kipa wa Marseille Elinton Andrade alilikubalia kutikisa wavu, baada ya kushindwa kulidhibiti vyema. Gomez karibu afunge la pili kwa kusukuma mkwaji karibu na lango katika dakika ya 59 lakini Andrade akaupangua, huku naye kipa wa Bayern Manuel Neuer upande ule mwingine wa uwanja akiokoa mkwaju wake mshambuliaji wa Marseille Loic Remy.

Bayern wana matumaini ya kucheza fainali katika uwanja wao wa nyumbani Allianz Arena
Bayern wana matumaini ya kucheza fainali katika uwanja wao wa nyumbani Allianz ArenaPicha: dapd

Lakini Bayern walijipa bao la pili la afueni wakati Robben alipocheza gonga nipe gonga nikupe na mwenzake Thomas Mueller kabla ya kuweka wavuni bao safi lililombwaga kipa Andrade. Kisha vijana hao wa kocha Jupp Heynckes wakachukua udhibiti kuanzia hapo hadi mwisho.

Schweinsteiger kukosa mchuano wa marudiano

Akizungumza baada ya mchuano kocha Heynckes alisema kitu cha pekee ambacho hakikuwa kizuri kwao ni kwamba walipata kadi za njano. Moja ilimwendea mchezaji wa akiba Bastian Schweinsteiger ambaye sasa hatacheza katika mchuano wa marudiano. Naye Robben alisema wangali na mchuano mmoja wa kucheza nyumbani Allianz Arena. Aliongeza kuwa mchezo wao ulikuwa mzuri pamoja na matokeo na sasa kuna uwezekano wa wao kukutana na Real Madrid katika nusu fainali.

Mario Gomez sasa anapungukiwa goli moja tu nyuma ya Lionel Messi aliyedhibitiwa vikali na AC Milan katika mchuano mkali ulioishia sare ya bila kufungana mjini Milan uwanjani San Siro, mchuano ambao pande zote mbili zilikuwa na nafasi nzuri za kufunga lakini hazikuzitumia vyema.

Barcelona watokwa jasho Milan

Zlatan Ibrahimovich alikuwa na nafasi ya wazi kwa upande wa AC Milan baada ya dakika 20 wakati alipoipata pasi yake Clerence Seedorf lakini mkwaju wake hafifu mshambuliaji huyo ukaokolewa langoni na kipa wa Barcelona Victor Valdes.

Lionel Messi alijaribu kuisumbua ngome ya Milan bila mafanikio
Lionel Messi alijaribu kuisumbua ngome ya Milan bila mafanikioPicha: dapd

Barcelona waliumiliki mpira kw akiwango kikubwa lakini walikuwa na matatizo ya kufanya mashambulizi yoyote katika lango la adui Milan ambao walikuwa wamejpanga vyema katika safu yake ya ulinzi, hadi dakika za mwisho wakati vijana hao wa kocha Pep Guardiola walipokaribia mara mbili kupata bao.

Carles Puyol alipiga kichwa juu ya lango kutoka mkwaju wa konakatika dakikay a78 nao mkwaju wa Messi ukaokolewa langoni na kipa wa Milan Christian Abiatti, dakika mbili mchuano kukamilika, huku naye Cristian Tello akasukuma shuti lililozuiwa.

Barcelona kuamua Camp Nou

Messi ambaye alikuwa mchezaji wa kwanza kuwahi kufunga magoli matano katika mchuano mmoja wa ligi ya mabingwa, wakati Barca ikiwazaba Bayer Leverkusen 7 – 1 katika awamu iliyopita, angali anahitaji goli la 50 la taaluma yake katika kinyang'anyiro cha Ligi ya Mabingwa. Lakini vijana hao wa Pep Guardiola wana fursa ya kufanya vyema katika mkondo wa pili uwanjani Camp Nou Jumanne ijayo. Mshindi atakutana na Chelsea au Benfica katika nusu fainali, huku klabu hiyo ya Premier League ikiongoza kufuatia ushindi wao wa moja sifuri mjini Lisbon siku ya Jumanne.

Kipa wa Barca Victor Valdes amesema walikuwa na nafasi nyingi lakini hawakuzitumia vyema. Kwamba walijaribu kupokezana pasi fupi wakati wakiumiliki mpira kwa muda mrefu. Anasema mchuano bado ni wazi na sas autaamuliwa uwanjani mwao.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA

Mhariri: Oummilkheir Hamidou