1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich haijakaa sawa baada ya Ancelotti

Sekione Kitojo
2 Oktoba 2017

Bayern bado haijakaa vizuri, baada ya kufutwa kazi kocha wake mkuu Carlo Ancelotti wiki  iliyopita, yaambulia sare na Hertha Berlin. Borussia Dortmund bado ngangari licha ya ushindi wa kibarua kikali dhidi ya Augsburg.

https://p.dw.com/p/2l7L9
Bundesliga 7. Spieltag - Hertha Berlin vs Bayern München - Niederlage des FC - Hummels
Picha: Getty Images/Bongarts/M. Rose

Willy Sagnol hakutaka  kufanya  makosa. Lakini  kocha huyo wa  mpito  wa  mabingwa  watetezi  wa  Bundesliga Bayern Munich  katika  mchezo  dhidi  ya  Hertha  BSC Berlin  alishindwa  kuhimili  vishindo  vya  wenyeji  na kupoteza  uongozi  wa  mabao 2-0 na  hatimaye  kuridhika na  suluhu  ya  mabao 2-2 , ikiwa  ni  mara  ya  pili  kwa Bayern  kufanya  hivyo katika  muda  wa  wiki  mbili.

Mshambuliaji  wa  Bayern Munich  Thomas Mueller  alikuwa na  haya  ya  kusema.

Bundesliga 7. Spieltag - Hertha Berlin vs Bayern München -  0:2 Tor
Wachezaji wa Bayern Frank Ribery (kushoto) na Lewandowski (kulia)Picha: Reuters/A. Schmidt

"Tumefadhaishwa sana  na  kuvunjika  moyo, kwamba  kwa mara  ya  pili  hatukuweza , kulinda  uongozi wetu  wa mabao 2 na  kuwa  ushindi  mwishoni."

Kocha wa  mpito Willy Sagnol  amelalamika  kwamba , walihitaji  katika  mchezo  huo  wachezaji  ambao  wako katika  hali nzuri  kimchezo baada  ya  mchezo  dhidi  ya Paris Saint Germain  katikati  ya  wiki  iliyopita  kwa  kuwa mchezo  huo  ulikuwa  mgumu na baadhi  ya  wachezaji walikuwa  wamechoka.

Na  pia mvutano  wa  kuwania  madaraka  chini  ya uongozi  wa  Ancelotti ulileta  athari kubwa katika  timu.

Mchezaji wa  ulinzi wa Hertha Berlin Niklas Stark  anasema.

Bundesliga 7. Spieltag - Hertha Berlin vs Bayern München -  2:2 Tor
Wachezaji wa Hertha Berlin wakifurahia bao la kusawazisha dhidi ya Bayern pamoja na mfungaji Salomon Kalou(katikati)Picha: Imago/Voigt/J. Huebner

"Tumepata pointi  moja. Kwasababu  unapokuwa  nyuma kwa  mabao 2-0 dhidi  ya  Bayern, ni rahisi  kukubali kushindwa."

Borussia  Dortmund imeshikilia  uongozi  wa  ligi  ya Bundesliga  ikiwa  na  pointi  19 na  mabao  21, wakati Bayern  Munich  kwa  kutoka  sare  na  Hertha Berlin imechupa  hadi  nafasi  ya  pili  ikiwa  na  pointi 14  pointi 5 nyuma ya  Dortmund.

TSG Hoffenheim  imeteremka  hadi nafasi  ya  tatu  kutokana  na  kipigo  cha  mabao 3-2 jana Jumapili  dhidi  ya  FC Freiburg. Florian Niederlechner mshambuliaji  wa  Freiburg anazungumzia  mchezo  huo.

"Ni  hali ya  kusisimua sana. Tumeonesha  mchezo  mzuri katika  michezo  yetu  miwili  iliyopita, lakini kwa  bahati mbaya  hatukuweza  kufaidika. Kwa bahati  nzuri  leo tumefanikiwa. Ni muhimu  sana. Pointi zetu tatu za  kwanza , kila  mtu  anatambua  sasa  kuwa  kikosi  chetu kiko hai."

FC Kolon  haijaanza  vizuri  msimu  huu  na  hadi  sasa hakujapatikana  jibu  mjarabu  kuhusu  masaibu yanayokikumba  kikosi  cha  kocha  Peter Stoeger.

Fußball Augsburg Deutschland 09 09 2017 1 Bundesliga 3 Spieltag FC Augsburg 1 FC Köln Trainer Stöger
Kocha wa FC Kolon Peter StoegerPicha: Imago/DeFodi/P. Fastl

Lakini  mwenyewe  bado  ana  matumaini.

"Kwangu  mimi  inatia  moyo, kuona  vijana  wangu  wana mwelekeo  sahihi, kuhusiana  na  kila  mara tunachowaambia. Nikiangalia  kwa  undani , wamefadhaika , na  vipi wanavyolalamika,  naona  hali  ni  ngumu, kuweza kubadilisha  hali  hiyo moja  kwa  moja."

FC Kolon  ina  pointi  moja  tu  na  inasubiri  kwa  hamu ushindi  wake  wa  kwanza  katika msimu  huu  wa  ligi  ya Bundesliga  na  inashika  mkia  baada  ya  michezo  7.

Bundesliga 7. Spieltag - Hertha Berlin vs Bayern München - Verletzung Ribery
Frank Ribery akisaidiwa kutoka nje baada ya kuumia mguuPicha: picture alliance/dpa/M. Kappeler

Wakati  huo  huo  Bayern Munich inatarajia  kukosa huduma  ya  mshambuliaji  wa  pembeni  wa  siku  nyingi Frank Ribery kwa  zaidi  ya  miezi  mitatu kutokana  na kukatika kwa  misipa  katika  goti  lake la  mguu  wa kushoto.Ribery mwenye umri wa  miaka  34 alisaidiwa wakati  akitoka  nje ya  uwanja  katika  mchezo  ambao Bayern ilitoka  sare  ya mabao 2-2  dhidi  ya  Hertha Berlin.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre / afpe / ape

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman