1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich na Olympique Lyon Leo

27 Aprili 2010

Champions League-nani ataingia finali ?

https://p.dw.com/p/N7xK
B.Munich leo bila RibberyPicha: AP

Katika duru ya pili ya nusu-finali ya champions league-Kombe la Klabu Bingwa barani ulaya,Bayern Munich ya Ujerumani, inateremka uwanjani leo usiku kutetea bao lake 1:0 iliotia katika duru ya kwanza nyumbani mjini Munich.Mahasimu wao katika kinyan'ganyiri hiki cha kukata tiketi ya finali ni Olympique Lyon,ya Ufaransa.

Kesho itakua zamu ya nusu-finali ya pili kati ya mabingwa FC Barcelona na mabingwa mara 6 wa Kombe hilo Inter Milan ya Itali.Inter, iliwanyoa mabingwa hao wa Spain bila ya maji katika duru ya kwanza huko Milan, ilipowazaba pamoja na stadi wao Lionel Messi, mabao 3:1.

Katika mpambano wa leo usiku kati ya Bayern Munich na Olympique Lyon,huko Lyon,Ufaransa, Bayern Munich, itamtegemea tena jogoo lake kutoka Holland, Arjen Robben, kuwika.Robben, ndie dawa mujarabu kwao . Mabao yake kadhaa aliowatilia kimiyani katika champions league, yatazamiwa kuziba pengo la udhaifu walio nao katika ulinzi tangu kuumia Muargentina, Martin Demichellis na mbelgiji Daniel Van Buyten na hata Diego Contento.Wote hao, kuna shaka kuweza kucheza leo.

Alikuwa Robben, alielifumania lango la Lyon mjini Munich katika duru ya kwanza na kuweka hayi matumaini ya Bayern Munich, ya klucheza finali ya champions League msimu huu na hasa baada ya kuipiga kumbo Manchester United.

Lyon , ambayo kamwe haikuwahi kufika nusu-finali ya champions league hapo kabla, ilifanya madhambi mengi ya kutotia bao kwa ukosefu wa maarifa ya kutosha katika duru ya kwanza mjini Munich.Wame waahidi kwahivyo, mashabiki wao kufuta madhambi yao hii leo.

Bayern Munich inaania vikombe 3 msimu huu,nyumbani inaongoza kwa magoli Bundesliga kati yake na Schalke na imeshakata tiketi ya finali ya Kombe la Ujerumani.Jumamosi lakini iliteleza na kupoteza pointi 2 kwa Borussia Moenchengladbach.

Msukosuko mwengine unasubiriwa kesho mjini Barcelona, ambako mabingwa wa Ulaya na Spain FC Barcelona,wanatumai jogoo lao kutoka Argentina, Lionel Messi, litafuta mabao 3L:1 ya Inter Milan katika duru ya kwanza.Kwa mabao hayo 3, kikosi cha Jose Mourinho kimeshatia mguu mmoja katika finali na leo kina azma ya kutia mgu wapili.

Umati wa mashabiki laki 1 utajkuwa uwanjani Nou camp kumuona Messi na Zlatan Ibrahimovic wakiifufua Barcelona. Itakuwa azma ya Inter Milan ,mabingwa mara 6 wa ulaya kuwazika kaburini nyumbani mwao.Barcelona ilitoka sare 0:0 nyumbani na Milan katika hatua kama hii ya nusu-finali miaka 4 iliopita,lakini mwishoe, ikatamba hadi finali na kutwaa taji.

Macho yote yatakodolewa kwahivyo, Lionel Messi, aliepachika hadi sasa mabao 17 katika mapambano 22 ya kombe hili msimu huu na uliopita.Msimu uliopita, aliibuka mtiaji mabao mengi katika Champiopns League.Kwahivyo,Inter Milan inakibarua kigumu kutetea mabao yake 3:1 ya duru iliopita.

Mwandishi: Ramadhan Ali/RTRE

Mhariri: Abdul-Rahman