1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michuano ya makundi ya Champions League yarejea

19 Oktoba 2015

Bayern Munich wanaendelea kupepea na kesho watashuka dimbani na Arsenal katika Champions League, lakini wenzao wa Bundesliga Bayer Leverkusen, Wolfsburg na Borussia Moenchengladbach wote wanakabiliwa na shinikizo.

https://p.dw.com/p/1Gqc7
Fußball Bundesliga FC Bayern München vs. BVB Borussia Dortmund
Picha: Reuters/M. Rehle

Kocha wa Arsenal Arsene Wenger amesema ni wakati wa kuamka kutoka usingizini. "Ni mpambano tunaotaka kushinda kwa sababu ndio mchuano wetu unaofuata. Naamini pia kuwa tunapaswa kuimarika barani Ulaya kwa sababu hatujawa katika kiwango chetu bora katika michuano miwili ya kwanza. Tumelenga zaidi Ligi ya Premier kuliko Ulaya. Tunafahamu katika mpambano huu lengo letu linapaswa kuwa sawa na lile la ligi ya PREMIER"-

Leverkusen watawaalika AS Roma kesho katika mchuano wa Kundi E wakifahamu kuwa kichapo kitawafanya wabanduliwe nje. Roma watawaruka Leverkusen na kusonga katika nafasi ya pili ikiwa watashinda, na kutaraji kuwa Barcelona watawabwaga BATE Borisov nchini Belarus.

Fußball Bundesliga 9. Spieltag Hamburger SV Bayer Leverkusen
Matatizo ya Leverkusen yamekuwa ni kufunga magoliPicha: picture-alliance/dpa/C. Charisius

Siku ya Jumatano, Gladbach inayoshikilia mkia itajaribu kupata pointi zake za kwanza katika Kundi D itakapomenyana na Juventus. Siku hiyo hiyo, Wolfsburg itaikaribisha PSV Eindhoven katika Kundi gumu kabisa la B ambalo lina timu zote pamoja na Manchester United na CSKA Moscow na pointi tatu. Sevilla watakuwa wageni wa Manchester City.

Mchuano mwingine ni kati ya Olympiacos dhidi ya Dinamo Zagreb. Chelsea watashuka dimbani dhidi ya Dynamo Kiev wakati Porto wakiwakaribisha Maccabi Tel Aviv katika mpambamo mwingine wa Kundi G.

Hapo kesho, nambari mbili Valencia watakuwa nyumbani kwa nambari tatu Gent katika Kundi H. Zenit St Petersburg watawaalika Lyon katika mpambano mwingine.

Siku ya Jumatano, viongozi wa Kundi A Real Madrid wataumana na Paris Saint-Germain ambao wana pointi sita sawa na Madrid, wakati Malmo na Shakhtar ambao hawajapata pointi zozote wakikutana nchini Sweden.

Pia siku ya Jumatano, Atletico Madrid watawaalika Astana katika Kundi C. Atletico wako katika nafasi ya pili katika kundi hilo, pointi tatu nyuma ya viongozi Benfica ambao watacheza ugenini Uturuki nyumbani kwa Galatasaaray.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu