1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yatota, Gladbach yapaa, yaiwinda Dortmund

Sekione Kitojo
26 Novemba 2018

Borussoa Moenchengladbach yasogea katika nafasi ya pili katika Bundesliga  ikiiwinda Borussia Dortmund, Bayern Munich yatota, majdala kuhusu kocha Nico Kovac wapamba moto kuna minong'ono  ya jina la  Arsene Wenger.

https://p.dw.com/p/38vqw
Fussball Bundesliga l Borussia Mönchengladbach vs Hannover 96 - Tor 2:1
Picha: Getty Images/Bongarts/M. Hitij

Borussia  Moenchengladbach  imerejea  katika  nafasi  yake  ya  pili katika  msimamo  wa  ligi  ya  Ujerumani Bundesliga  jana  kwa kuonesha  mchezo  mwingine  mzuri  wa  kushambulia  na  kuichapa Hannover  kwa  mabao 4-1.

Fussball Bundesliga l Borussia Mönchengladbach vs Hannover 96 – Tor 1:1
Wachezaji wa Borussia Moenchengladbach wakifurahia kwa pamoja ushindi dhidi ya Hannover 96Picha: Getty Images/Bongarts/M. Hitij

Ni viongozi  wa  ligi  hiyo  tu  Borussia  Dortmund  ambayo imezisalimia  mara  nyingi  nyavu  za  adui , ikiwa  imeweka  wavuni mabao  35  katika  michezo 12  ya  ligi  msimu  huu, wakati Gladbach  imefikisha  mabao 30 licha  ya  kuanza  mpambano  wa jana  kwa  kuwa  nyuma  kwa  bao  moja  katika  sekunde  ya  12 tangu  mchezo huo  kuanza. 

Mshambuliaji  kutoka  Marekani  Bobby Wood aliweka  wavuni bao safi sekunde  chache  baada  ya  kuanza  mchezo kwa  Hannover na kutimiza  bao  lake  la  tatu  msimu  huu. Wakati  huo hakuna mchezaji  wa  Gladbach  aliyeugusa  mpira.

Mchezo  huo  hata  hivyo uliingia  dosari  baada  ya  mlinzi  wa Gladbach  Matthias Ginter kugongana  na  Noah Joel Sarenren Bazee wa  Hannover. Baada  ya  kupatiwa  matibabu  uwanjani Ginter  aliondolewa  uwanjani  hapo  kwa  machela  na  kupelekwa hospitali. Taarifa  zinasema  kuwa  mchezaji  huyo  wa  timu  ya  taifa ya  Ujerumani  pia  hataweza  tena  kucheza  katika  mwaka  huu  wa 2018 . Mchezaji  huyo  ameumia  katika  sehemu  ya  jicho  lake pamoja  na  mfupa wa  shavu.

Fussball Bundesliga l Borussia Mönchengladbach vs Hannover 96 - Ginter und Sarenren-Bazee
Wachezaji wawili Matthias Ginter wa Gladbach na Bazee wa Hannover wakiwa chini baada ya kugonganaPicha: picture alliance/dpa/M. Becker

Bayern yatumbukia katika matatizo

Werder Bremen  imefikisha  mwisho  mfululizo  wa  michezo  mitatu bila  ushindi  kwa  kutoka  sare  ya  bao 1-1  jana  Jumapili  dhidi  ya Freiburg. Hata  hivyo  Bremen inabakia  katika  nafasi  ya saba katika  msimamo  wa  ligi  ya  Ujerumani.

Bayern Munich imetumbikia  katika hali  ngumu  msimu  huu  baada ya  kutopata  matokeo  mazuri  katika  ligi  kwa  zaidi  ya  michezo minne, na  iko  nyuma  ya  Borussia  Dortmund  inayoongoza  ligi hiyo  kwa  pointi  tisa. Bila  shaka  hili  si  jambo  la  kawaida  kwa vigogo  hao  wa  soka  nchini  Ujerumani, lakini  baada  ya  kutoka sare  ya  mabao 3-3  dhidi  ya  timu  iliyopanda  daraja  msimu  huu Fortuna  Dusseldorf nyumbani  katika  uwanja  wa  Alianz Arena, hali si  shwari  tena.

Deutschland Fußball Bundesliga FC Bayern München - Bayer 04 Leverkusen
Mshambuliaji wa Bayern Munich Arjen Robben akisikitika kutokana na matokeo dhidi ya Fortuna DusseldorfPicha: Bongarts/Getty Images/A. Hassenstein

Kocha  Nico  Kovac  anasema  ameumia  sana  kwa  matokeo hayo:

"Mnaweza  kufikiria  vile ninavyojisikia. Sifahamu  iwapo  hasira zinazidi  kupanda , kwasababu , wakati mchezo umekwisha udhibiti na  katika  dakika  za  mwisho  bao  linarejeshwa. Kwanza  tuliongoza kwa  mabao 2-0 na  kabla  ya  mapumziko  matokeo  yanakuwa  2-1. Tuliongoza  tena  kwa  mabao 3-1 na  kisha  katika  dakika  ya  92 inakuwa  3-3. Siwezi kuwa  na  furaha, na  nimekasirika  sana  na naelewa  kuhusu  uwezo  wetu wa  kujilinda  ambao  hatukuweza kuutumia, kibaya  zaidi ni  jinsi tulivyojilinda  wakati  tunafungwa  bao la  tatu."

Honnes amkingia  kifua Kovac

Hata  hivyo  kocha  wa  Furtuna  Dusseldorf Friedel Funkel amesema amefarijika  sana  kuona  timu  yake  ilivyopambana  katika  uwanja wa  ugenini  mjini  Munich  na  kupata  sare  hiyo.

1. Bundesliga | Bayern München v Fortuna Düsseldorf | Hat-Trick-Torschütze Dodi Lukebakio
Mshambuliaji Dodi Lukebakio wa Fortuna DusseldorfPicha: picture-alliance/dpa/M. Balk

"Bila  shaka nimefurahi  sana kwamba  kabla  ya  firimbi  ya  mwisho ya  mchezo tuliweza  kupachika  bao la  kusawazisha. Na  hii ikiwa baada  ya  kuwa  nyuma  kwa  mabao  mawili, lakini  hatukupoteza mwelekeo  wetu. Tuliendelea  kulinda lango  letu kwa  pamoja. Na iwapo Bayern  wangepata  bao la  4 kila  kitu  kingekuwa kimemalizika. Na tulikuwa  tu  na  matumaini  kwamba  hali  itakwenda vizuri kwetu, na  tungeweza  kufanya  vizuri kwa  kutumia  kasi  ya mshambuliaji  wetu Dodi Lukebakio."

Mjadala  mkali  unaendelea  hivi  sasa  kuhusu  kocha  Nico  Kovac, kutokana  na  matokeo  hayo  mabaya  kwa  Bayern Munich. Kuna majina  kadhaa  yanayotajwa  , lakini  vyombo  vya  habari  za michezo  nchini  Ujerumani zinajaribu  kuibua  minong'ono  ya  majina kama Arsene Wenger  kocha  wa  zamani  wa  Arsenal  London.

Fußball Bundesliga l Hertha BSC Berlin vs Bayern München 2:0 l Trainer Nico Kovac
Kocha wa Bayern Munich Nico KovacPicha: Getty Images/Bongarts/B. Streubel

Huyu  anafikiriwa  huenda  akachukua  nafasi  ya  Nico  Kovac  kwa kuwa  Bayern  inahitaji  kocha  mwenye jina  kubwa  katika  medani ya  soka,  na  pia  mwenye  uzoefu. Piam  kuna  jina  la  Ralph Hasenhuetel , aliyekuwa  kocha  wa  zamani  wa  RB Leipzig  ya Ujerumani  na  pia Mark van Bommel  kocha  wa  sasa  wa  PSV Eidhoven. hata  hivyo  rais  wa  Bayern  Munich  Uli  Honness anamkingia  kifua  Nico  Kovac kwa  kusema.

"Timu ilicheza  kwa   tahadhari  sana  katika  kipindi  cha  kwanza  na pia  kwa  upande  wa  kasi, hatujacheza  kama  ilivyotarajiwa. Lakini kipindi  cha  pili timu  ilianza  kujiamini  zaidi  na  nadhani  katika kipindi  cha  pili  timu  ilicheza  vizuri  zaidi."

Fortuna Düsseldorf - Düsseldorfs Trainer Friedhelm Funkel
Kocha wa Fortuna Dusseldorf Friedhelm FunkelPicha: picture-alliance/dpa/J. Güttler

Eintracht  Frankfurt imechupa  hadi  nafasi  ya  tatu  ya  msimamo wa  ligi, kwa  ushindi  wa  mabao 3-0  dhidi  ya  Augsburg , wakati RB Leipzig iliyoko  katika  nafasi  ya  nne  ilikwaa  kisiki  dhidi  ya Wolfsburg  kwa  kukubali  kipigo  cha  bao 1-0.

Bayern iko  nafasi  ya  nne ikifuatiwa  na  TSG Hoffenheim iliyotoka sare  na  Hertha Berlin  ya  mabao 3-3. Fortun a Dusseldorf licha  ya kutoka  sare  na  bayern Munich inashikilia  nafasi  ya  17 ikiwa  na pointi 9, ikiwa  katika  nafasi  ya  kushuka  daraja.

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe /rtre / ape / dpae

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman