1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bei ya chakula ulimwenguni imepanda wakati wa janga la COVID

Yusra Buwayhid
4 Desemba 2020

Bei ya chakula ulimwenguni imepanda kwa mwezi wa sita mfululizo, ikigonga kiwango cha juu kabisa tangu Desemba 2014, kulingana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO.

https://p.dw.com/p/3mCzw
Brasilien - Ernte Zuckerrohr
Picha: picture-alliance/dpa/W. Rudhart

Kulingana na shirika hilo la chakula la Umoja wa Mataifa, bei ya chakula imeongezeka mwezi Novemba kwa kiwango ambacho hakikuwahi kushuhudiwa kwa miaka sita.

Faharisi inayochapishwa kila mwezi na shirika hilo la FAO, hapo Alhamisi imedhihirisha kwamba bei za bidhaa kadhaa za chakula zimeongezeka mno mwezi Novemba.

Bidhaa ambayo imeongezeka bei zaidi ni mafuta ya kupikia. Kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta ya mawese, bei ya mafuta ya kupikia imeongezeka kwa asilimia 14.5.

Bei za vyakula vya nafaka, sukari, nyama, na maziwa pia zimeongezeka.

Kiwango cha bei ya sukari kiliongezeka kwa asilimia 3.3% kutokana na kupungua kwa uzalishaji ulimwenguni kote. Hali mbaya ya hewa imedhofisha mavuno katika mataifa ya Umoja wa Ulaya, Urusi na Thailand.

Sudan Bauer mit Mohrenhirse in Bulbul Dalal Angara, Nyala, Süd-DarfurA farmer is harvesting sorghum plants from seeds donated by the FAO (Food & Agriculture Organization) in Bulbul Dalal Angara region of Nyala, Southern Darfur, 1980 km west of Khartoum. British sci
Mkulima wa Sudan akivuna mtama mweusi huko Bulbul Dalal Angara, Nyala, Darfur KusiniPicha: picture-alliance/Photoshot/Lightroom Photos/F. Noy

Bei za mazao makuu ya nafaka zilipanda kwa wastani wa asilimia 2.5, ingawa bei zilikuwa zimepanda kwa asilimia 20 mwaka jana. Bei za nyama na maziwa hazukuongezeka sana.

Waliopoteza kipato kutokana na COVID-19 wameathrika zaidi

Shirika la FAO limesema ongezeko la bei za vyakula limewaathiri zaidi wale ambao kipato chao pia kimepungua kutokana na janga la virusi vya corona.

Ripoti ya shirika hilo imesema kwamba janga la ugonjwa wa COVID-19 limesababisha kuongezeka kwa viwango vya ukosefu wa chakula ulimwenguni.

Na kutaja kwamba, ilichofanya janga hilo ni kuchochea hali ambayo tangu hapo ilikuwa mbaya kutokana na migogoro mbalimbali ulimwenguni, mashambulizi ya wadudu kwenye mimea ya mazao, majanga asilia ikiwa ni pamoja na vibunga Amerika ya Kati na mafuriko barani Afrika.

Shirika la FAO limesema katika orodha ya nchi 45, 34 kati yao za barani Afrika, zinaendelea kuhitaji msaada wa kutoka nje kuweza kupata chakula cha kutosha.

Aidha shirika hilo limetaja sababu nyingine kuwa ni kunyesha kwa kiwango kikubwa cha mvua kisicho cha kawaida kusini mwa Afrika na Asia Mashariki. Wakati huo huo, katika sehemu za Asia ya Mashariki na Afrika Mashariki kulikuwa na matarajio ya kupungua kwa mvua. Hali zote mbili limesema shirika hilo la FAO zinaathiri uvunaji wa mazao.

Chanzo: afap