1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bei ya mafuta yashuka hadi dola 50 kwa pipa

14 Novemba 2008

Shirika la OPEC kukutana kuzingatia hali katika masoko.

https://p.dw.com/p/FuwP
Rais wa Shirika la nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi Chakib KhelilPicha: AP

Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema bei ya mafuta duniani inaweza ikashuka bila hadi dola 50 kwa pipa na hata kushuka zaidi hadi dola 40 au 35, lakini zinaweza kupata tena afuweni haraka.

Jana (Alhamisi) bei ya mafuta ilikua dola 55 za kimarekani, kiwango cha chini kuwahi kuonekana katika muda wa miezi 22 iliopita, kukitokeza dalili zinazoashiria hali mbaya ya kiuchumi itakua na athari kubwa katika upande wa mahitaji ya mafuta, ikipunguza matumizi ya mafuta viwandani na kwa watu wa kawaida.

Bei ya mafuata imeshuka asili mia 60 tangu yalipopanda mno mwezi Julai na kufikia dola 147 na senti 27 kwa pipa, lakini sasa inaelekea kwenye dola 50. Wachambuzi wengi wanaashiria bei itazidi kuanguka.

Kuanguka kwa bei ya mafuta katika masoko mnamo miezi minne iliopita, kunatokana na sababu kadhaa. Lilo wazi ni hali mbaya mno ya kiuchumi duniani, na wataalamu wanagusia zaidi juu ya kupungua mahitaji au kwa maneno mengine matumizi ya mafuta.

Shirika la nishati la kimataifa , International Energy Agency (IEA) linalozishauri nchi 28 za viwanda, jana lilitoa taarifa ya utafiti wake juu ya mtazamo wa ongezeko la mahitaji ya mafuta duniani.

Utafiti huo ulitaja kwamba mahitaji yameongezeka kawa kasi ndogo mwaka huu na mwaka ujao yanatarajiwa kuongezeka kwa kiwango cha mapipa 350.000 tu kwa siku.

Mahitaji ya mafuta duniani sasa yanatarajiwa kuwa katika kiwango cha mapipa 86.2 milioni kwa siku mwaka huu wa 2008, yakiongezeka hadi mapipa 86.5 tu milioni mwaka ujao 2009.

Kuanguka kwa kiwango cha mahitaji kimezusha hoja miongoni mwa wafanyabiashara ya mafuta kwamba masoko ya mafuta yatafurika bidhaa hiyo.

Shirika la nchi zinazotoa mafuta kwa wingi OPEC lilikubaliana mwezi uliopita kupunguza utoaji mafuta kwa mapipa milioni 1.5 kwa siku kuanzia tarehe 1 mwezi huu wa Novemba, huku wachambuzi wengi wa mambo wakifikiria huenda kiwango hicho kikapunguzwa zaidi.

Afisa mmoja anayehusika na masuala ya mafuta wa Iran amesema wanachama wa Shirika la OPEC watakutana mjini Cairo tarehe 29 mwezi huu, kushauriana kuhusiana na hali ya mambo katika masoko, hatua inayofikiriwa kuwa na lengo la kuzipa msukumo bei za mafuta zilizoanguka wakati huu.

Mtaalamu mmoja wa uchumi amesema hali katika soko inaweza ikaanza kubadilika, ikiwa Shirika la OPEC linalotoa karibu 40 asili mia ya mafuta ya dunia, litaamua kupunguza kiwango cha uchimbaji.

Wajumbe wa Umoja wa nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani (OPEC) wanatarajiwa kukutana mwishoni mwa mwezi huu katika kikao maalum kujadili kupungua kwa kasi bei ya mafuta yasiyosafishwa katika soko la dunia.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa OPEC, Shakib Khelil amesema wajumbe 13 wa umoja huo watakutana mjini Cairo-Misri kandoni mwa mkutano uliopangwa awali wa wajumbe wa nchi za Kiarabu wanachama wa Shirika la OPEC.

Bwana Khelil ambaye pia ni Waziri wa Nishati wa Algeria amesema leo kwamba mkutano huo utazingatia ni maamuzi gani yanapaswa kuchukuliwa.

Mnamo wiki iliopita Mwenyekiti huyo wa OPEC alisema angependelea kupunguzwa zaidi kiwango jumla cha utoaji mafuta, ikiwa uamuzi wa kupunguza mapipa milioni 1.5 uliopitishwa na umoja huo mwezi uliopita, hautoirejesha bei kuwa baina ya dola 70 na 90 kwa pipa.