1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIJING: Korea ya kaskazini yakubali kurejea kwenye mazungumzo na nchi 6 juu ya suala la kinyuklia

1 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCxA

Korea ya kaskazini imekubali kurejea kwenye mazungumzo na nchi 6 zenye nguvu za kinyuklia. Korea ya kaskazini imesema itaomba iondolewe hatua ya kuzuwiliwa kutumia benki za kigeni na kwamba makubaliano hayo juu ya mazungumzo kuhusu mpango wake wa kinyuklia, yamefikiwa baada ya mazungumzo ya ana kwa ana na wawakilishi wa Marekani nchini Uchina. Hatua ilichukuliwa katika mkutano na maafisa wakuu wa Korea ya kaskazini, Uchina na Merekani mjini Beijing.

Rais wa Marekani, George W. Bush, baada ya kusikia habari hiyo, ametangaza furaha yake kwa kuwapongeza wale wote waliochangia kufikia hatua hiyo:

´´Ninayo furaha. Na ningependa kuishukuru Uchina ambayo iliandaa mkutano huo ambao umefanikiwa kufikia kwenye makubaliano ya kufanyika tena mazungumzo na nchi 6. Kila mara nilihisi kuwa ni muhimu Marekani kuwa kwenye meza ya mazungumzo na washirika wenzetu linapokuja suala tete kama hilo. Kwa hiyo ninatoa shukrani sio tu kwa Uchina, bali pia kwa Korea ya kusini, Japan na Rushia kukubali kurudi kwenye meza ya mazungumzo na Korea ya kaskazini´´.

Kiongozi wa ujumbe wa Marekani kwenye mazungumzo hayo, Christopher Hill, amewaambia waandishi wa habari kwamba Korea ya kaskazini haikutoa masharti kabla ya kukubali kurudi kwenye mazungumzo hayo ambayo huenda yakaanza mwezi ujao.

Hatua hiyo imefikiwa wiki tatu baada ya Korea ya kaskazini kudai kuwa ilifanikiwa katika jaribio lake la kuripua bomu la kinyuklia. Korea ya kaskazini ilijotoa kwenye mazungumzo juu ya nyuklia mwaka moja uliopita ili kulalamika kuhusu vikwazo vya fedha ilivyowekewa na Marekani.