1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIRUT:Kadinali wa madhehebu ya Maronite kutangaza orodha ya wagombea wa urais

14 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CG1Q

Viongozi wa kisiasa nchini Lebanon wanamsubiri Kadinali wa Maronite aliye na ushawishi mkubwa kutangaza wagombea wa uraisi huku juhudi za kidiplomasia zikiimarishwa ili kumaliza mkwamo wa kisiasa.Kadinali Nasrallah Sfeir anayeongoza kanisa lililo na wafuasi wengi zaidi nchini humo anatarajiwa kutangaza orodha ya majina sita kabla muda wa mwisho wa Novemba 23 kuwadia.Rais wa Lebanon sharti atoke katika Jamii ya Kikristo ya Maronite kwa mujibu wa katiba na mfumo wa uongozi.

Wanadiplomasia kutoka mataifa ya magharibi wanatia juhudi kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa ili kuepuka vita vya wenyewe kwa wenyewe kama vilivyotokea mwaka ’75-90 pale pande mbili zilipongangania madaraka.

Spika wa Bunge Nabih Berri amelazimika kuahirisha mara tatu kikao maalum cha wabunge cha kumteua rais kwasababu ya kutoelewana kati ya chama tawala kilicho na wawakilishi wengi bungeni na upande wa vyama vya upinzani.Kikao cha bunge kinachopangwa kufanyika tarehe 21 mwezi huu aidha huenda kikashindwa kumtafuta mrithi wa Rais Emille Lahoud anayeungwa mkono na Syria.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Benard Kouchner alifanya mazungumzo hapo jana mjini Beirut huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akitarajiwa kuzuru Lebanon hapo kesho.Ufaransa iko mstari wa mbele katika juhudi za kidiplomasia za kutafuta suluhu ya mwakamo wa kisiasa.

Vyama vya upinzani vinatisha kutomtambua rais atakayeteuliwa na wingi wa kura pekee.Hatua hiyo huenda ikasababisha kuundwa kwa serikali mbili zinazonganania madaraka.

Lebanon inazongwa na matatizo ya kisiasa tangu kuuawa kwa waziri mkuu marehemu Rafiq Hariri mwaka 2005.