1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIT HANUN : Vilio na hasira vyatawala mazishi huko Gaza

10 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCuL

Maelfu ya Wapalestina wamelizana na kupiga mayowe ya kulipiza kisasi hapo jana wakati wakiwazika raia wao 18 waliouwawa huko Gaza kutokana na mashambulizi ya mizinga ya Israel ambayo Waziri wa Mkuu wa Israel amesema yametokana na makosa ya kiufundi ya mfumo wa silaha zao za mizinga.

Miongoni mwa waliouwawa ni watoto saba na wanawake wanne na aliekuwa na umri mdogo kabisa alikuwa ni msichana wa miezi 18 ambaye baba yake alimuanika hewani wakati wa maandamano ya maziko hayo katika mji wa Gaza ya kaskazini wa Beit Hanun ulioshambuliwa hapo Jumaatano na mizinga ya Israel.Wanawake kadhaa walizirai kwa huzuni na wapiganaji wa Kipalestina walikuwa wakifyatuwa risasi hewani.

Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert amesema ataendelea kuwashambulia wanamgambo wa Kipalestina wanaovurumisha maroketi nchini Israel kutokea Gaza licha ya kuhatarisha maisha ya raia bila ya kukusudia.

Akizungumza mjini Tel Aviv katika mkutano wa baiashara Olmert amesisitiza kuwa tayari kwake kukutana na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina kwa kusema kwamba kiongozi huyo wa Palestina atashangaa atakapoketi naye kwa namna walivyo tayari kujitolea kwa kiasi kikubwa katika kumaliza mzozo wa Israel na Palestina.

Waziri Mkuu huyo wa Israel hakufafanua zaidi.