1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bemba aubeza uchaguzi DRC baada ya kuondolewa

Iddi Ssessanga
5 Septemba 2018

Mbabe wa zamani wa kivita nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Jean-Pierre Bemba ameubeza uchaguzi wa rais unaofanyika Desemba kama maigizo, baada ya mahakama ya juu kumpiga marufuruku kushiriki. Mwanasiasa wa upinzani Monique Mukuna Mutombo alizungumza na John Juma kuhusu hatua hiyo ya kuzuwiwa kwa Bemba.

https://p.dw.com/p/34KVN

Bemba ni miongoni mwa wagombea sita ambao tume ya uchaguzi ilikata majina yao katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa urais unaopangwa kufanyika Desemba 23.  Alikuwa amekata rufaa kupinga uamuzi huo, lakini mahakama ya katiba ilithibitisha uamuzi huo katika hukumu ya Jumatatu jioni, na kusema aliondolewa kutokana na kutiwa hatiani na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC kwa kuwahonga mashahidi aktika kesi yake ya uhalifu wa kivita.

"Ukweli kwamba mtu anachagua wapinzani --- inatia wasiwasi mkubwa," Bemba aliiambia televisheni ya France 24, na kuongeza kuwa taifa hilo linalokumbwa na machafuko ya mara kwa mara litashuhudia "igizo la uchaguzi." Koloni hilo la zamani la Ubelgiji halijashuhudia mabadiliko ya amani ya utawala tangu 1960.

Rais Joseph Kabila, ambaye amekuwa madarakani tangu 2001, hatimaye alisema hatowania tena baada ya kukaa kimya kuhusu suala hilo kwa miezi kadhaa na kuchochea wasiwasi na machafuko mabaya katika taifa hilo tete. Mhula wa pili na wa mwisho wa Kabila ulikamilika miaka miwili iliyopita. Baadi ya wataalamu wanahofia nchi hiyo kutumbukia katika umuagaji damu.

Internationaler Strafgerichtshof Jean-Pierre Bemba
Jean-Pierre Bemba akiwa katika chumba cha mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC mjini The Hague, Uholanzi, Machi 21, 2016 akisubiri kutolewa hukmu katika kesi dhidi yake.Picha: picture-alliance/dpa/J. Lampen

Bemba alitangaza nia yake ya kugombea baada ya kurejea kwa ushindi nyumbani akitokea Ubelgiji, ambapo mamia kwa maelfu ya wafuasi wake walijitokeza kumlaki, baada ya mahakama ya ICC iliyoko mjini The Hague, kumfutia mashitaka ya uhalifu wa kivita.

Hatia ya kuwahonga mashahidi

Mwezi Juni, jopo lililogawika pakubwa ya majaji watano wa ICC, lilibatilisha hatia ya mwaka 2016 dhidi ya Bemba, pamoja na kifungo cha miaka 18 gerezani kwa makosa ya uhalifu wa kivita dhidi ya ubinadamu, yaliodaiwa kufanywa na wanajeshi wake katika nchi jirani ya Jmahuri ya Afrika ya Kati mnamo mwaka wa 2003.

Hata hivyo, Bemba na watuhumiwa wenzake watano walitiwa hatiani katika rufaa ya kutoa hongo, rushwa na kuwafunza cha kusema mashahidi 14 wa upande wa utetezi katika kesi yake kuu. Baadae mwezi huu wa Septemba, mahakama hiyo ya kimataifa itamhukumu makamu huyo wa zamani wa rais kwa kuwahonga mashahidi.

Kabila ambaye alichukuwa madaraka baada ya kuuawa kwa baba yake, Laurent-Desire Kabila na mlinzi wake, ni hasimu mkubwa wa Bemba. Mhula wa Kabila katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali umechafuliwa na madai ya kukithiri kw arushwa, ukosefu wa usawa na machafuko.

Bemba alishindwa na Kabila katika uchaguzi wa rais wa 2006 na baadae alituhumiwa kwa uhaini, wakati walinzi wake walipopambana na jeshi mjini Kinshasa. Mwaka 2007, alikimbilia nchini Ubelgiji, ambako aliishi kwa sehemu ya ujana wake. Baadae alikamatwa barani Ulaya kwa waranti wa ICC kwa uhalifu wa kivita uliofanywa na jeshi lake binafsi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kuanzia 2002-3, wakati rais wake wa waakti huo Ange-Felix Patasse alipotafuta msaada wa kuzima jaribio la mapinduzi.

DR Kongo Wahlkampf in Kinshasa
Wafuasi wa chama cha MLC chake Jean-Pierre Bemba wakimsubiri kwa hamu Julai 30, 2018, kurejea nchini baada ya kutokuwepo nchini humo kwa muda wa miaka 11.Picha: Getty Images/AFP/J.D. Kannah

Mwanzo na uasi na kuundwa kwa kundi la MLC

Bemba, ambaye aliteuliwa kuwa makamu wa rais katika serikali ya mpito kuanzia 2003 hadi 2006, alizaliwa Novemba 4, 1962, katika eneo la Bogada, mkoa wa Equatuer uliyoko kaskazini-magharibi. Baba yake alikuwa mfanyabiashara tajiri mwenye ukaribu na dikteta Mobutu Sese Seko, alietawala kuanzia 1965 hadi alipopinduliwa mwaka 1997. 

Bemba alichukuwa uendeshaji wa biashara ya familia, akitumia umaarufu wake mjini Kinshasa kujengea kwenye utajiri wake na kupanua wigo katika sekta nyingine kama vile simu za mkononi, uchukuzi wa mizigo kwa ndege na televisheni. Aliondoka nchini Congo mwaka 1997 baada ya Laurent-Desire kumuondoa Mobutu. Mwaka mmoja baadae kulitokea vita vilivyodumu hadi 2003 na kuvutia uungaji mkono wa mataifa ya kigeni kwa pande hasimu.    
      
Bemba alikuja kuwa kiongozi wa kundi la waasi la Congolese Liberation Movement MLC, ambalo lilikuwa na wanajeshi 1,500 wakiungwa mkono na nchi jirani ya Uganda na likipambana dhidi ya utawala wa Kabila. MLC, ambayo sasa ni chama cha siasa, kiliitaka ICC siku ya Jumanne itoe uamuzi wake kwa sababu Bemba amezuwiwa isivyo haki na mahakama ya katiba ya Congo.

Baada ya kumalizika kwa vita vya Congo mwaka 2003, Bemba aliweka chini silaha na alitunukiwa mmoja ya nafasi nne za makamu wa rais zilizogawanwa katika serikali ya mpito miongoni mwa mahasimu wa wakati wa vita.  Bemba mwenye mwili mkubwa na urefu wa futi 6 na inchi 3, amepewa majina la utani ya "Chairman" na "Maniature Mobutu" kutokana na haiba yake kibabe.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri: Yusra Buwayhid