1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki kuu ya Marekani yainusuru AIG

Kalyango Siraj17 Septemba 2008

Mgogoro watishia maelfu kadhaa kupoteza ajira London

https://p.dw.com/p/FK5b
Mwanamme moja akitoka katika ofisi za jengo la shirika la Bima la Marekani la American International Group New York.Picha: AP

Benki kuu ya Marekani imetangaza kuwa imetoa mkopo wa dola za kimarekani billioni 85 kwa shirika la bima la Marekani AIG kama njia za kulinusuru kufilisika.

Habari za kufilisika kwa shirika la bima la Marekani zimesababisha hofu katika masoko ya hisa barani Ulaya pamoja na Asia.Lakini taarifa kutoka Afrika kusini zinasema kuwa nchi hiyo itahimili vishindo vya mgogoro wa sasa.

Tangazo la Benki kuu ya Marekani la kulipiga jeki shirika la Bima la Marekani la American International Groug AIG limesaidia kutuliza wasiwasi ulikuwepo.

Mpango wa benki hiyo unaipa serikali ya Marekani uwezo wa kumiliki asili mia 80 ya shirika hilo.

Rais George W Bush ameunga mkono hatua ya benki hiyo.Katika taarifa iliotolewa na Ikulu ya Marekani, rais Bush amenukuliwa kusema kuwa hatua hii imechukuliwa kutokana na kile kilichoitwa kuimarisha masoko ya fedha na pia kupunguza hasara iliokuwa inakabilia uchumi kwa ujumla.

Benki kuu ya Marekani hapo awali ilikuwa pia imeipiga jeki sekta ya masoko ya fedha kwa lengo la kupunguza wasiwasi uliosababishwa jumatatu na kuporomoka kwa benki ya Lehman Brothers.

Kuporomoka kwa benki ya Lehman pamoja na tisho la kuporomoka kwa shirika la bima la AIG ambalo ndilo kubwa kuliko yote nchini humo vilileta wasiwasi katika masoko ya hisa na ya fedha hapa Ulaya pamoja na Asia.

Masoko ya Ulaya yalipata kijibaridi pale iliporipotiwa kuwa Benki moja ya Uingereza Lloyds TBS ilikuwa inafanya majadiliano ya kuichukua benki ambayo imekuwa inajihusisha na mikopo ya nyumba ya Halifax Bank of Scotland-HBOS ambayo nayo inakabiliwa na matatizo katika soko la hisa.

Wasemaji wa benki hizo mbili za Uingereza,Lloyds TBS na HBOS, wamekataa kusema lolote kuhusu taarifa hizo ingawa habari zenyewe zimesaidia kupandisha bei ya hisa za HBOS.

Awali mawaziri pamoja na wachambuzi walikuwa wameonya kuwa uchumi wa bara la Ulaya utaumia kutokana na mgogoro wa fedha unaoendelea japo athari kamili baado hazijajulikana.

Kuna hofu kuwa huenda watu maelfu kadhaa katika jiji la London wakapoteza ajira zao kutokana na mgogoro huu.

Waziri wa fedha wa Luxemburg-Jean-Claude Junker amesema kuwa haamini ikiwa kile kinachoendelea kitasaidia maendeleo yoyote kutokana na wasiwasi uliopo.

Waziri huyo alikuwa anazungumza mjini Brussels kwa niaba ya mawaziri wa fedha wa mataifa 15 ya Ulaya yanayotumia sarafu ya Euro.Alikuwa anatumia kofia yake kama mwenyekiti wa mikutano yao ya kila mara.

Katika bara la Asia benki kuu za kanda hiyo zimekuwa zikimimina pesa katika soka la fedha ili kuhakikisha kuwa wafanya biashara wanapata pesa za kutosha kuendesha biashara zao.

Mfano benki kuu ya Japan inaripotiwa imeweka dola za kimarekani takriban billioni 51.8.

Na barani Afrika mambo hayatakuwa mabaya sana kwa soko la fedha la Afrika kusini, nchi ambayo inachukuliwa kuwa na uchumi bora kuliko mataifa yote barani humo.

Mkurugenzi mkuu wa Hazina ya Afrika kusini Lesetja Kganyago amenukuliwa kusema kuwa ingawa uchumi wa nchi hiyo utasumbuliwa na mgogoro wa sasa hata hivyo usumbufu hautakuwa mkali wa kuifanya serikali kuweza kuingilia kati.

Afisa huyo ameongeza kuwa hii ni kutokana na utaratibu wa kinga uliowekwa na serikali.