1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki ya Dunia kuudhamini Mradi wa Inga

Admin.WagnerD21 Machi 2014

Benki ya Dunia imeridhia kutoa dola milioni 73 kuisaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mpango wake wa ujenzi wa bwawa la Inga, ambalo ndilo kubwa kabisa duniani la kuzalisha umeme kutumia nguvu ya maji.

https://p.dw.com/p/1BTiu
Mitambo mikongwe kwenye bwawa la Inga ambalo Benki ya Dunia imekubali kulidhamini
Mitambo mikongwe kwenye bwawa la Inga ambalo Benki ya Dunia imekubali kulidhaminiPicha: DW

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Benki ya Dunia, fedha hizo dola milioni 73 zikichanganywa na zengine dola milioni 33 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika, zitasaidia kufadhili utafiti wa kiufundi kuchunguza hali ya mazingira karibu na eneo la bwawa na kuhakikisha mradi huo ni endelevu.

Fedha hizo pia zitasaidia kuzindua usimamizi wa maendeleo ya Inga unaojitegemea ambao unatarajiwa kufuata mfumo mzuri wa Kimataifa katika kuuendesha mradi huo, na hata kuteua mashirika binafsi yatakayosaidia katika kuufadhili zaidi mradi wa bwawa la Inga.

Hata hivyo, Benki ya Duinia imeiorodhesha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kama moja ya maeneo 10 yaliyo magumu kufanyia biashara. Kwa miongo kadhaa sasa miradi ya kulipanua bwawa hilo la Inga imeshidnwa kutokana na migogoro na vita vinavyotokea mara kwa mara nchini humo, huku wanamazingira wakionya kuwa mipango ya mabwawa makubwa inajulikana kwa kucheleweshwa kwa muda mrefu na kuwa na gharama kubwa.

Bwawa la kuzalisha umeme la Inga ndilo kubwa zaidi duniani
Bwawa la kuzalisha umeme la Inga ndilo kubwa zaidi dunianiPicha: ISSOUF SANOGO/AFP/Getty Images

Benki ya Dunia inakadiria kuwa Kongo itakuwa na uwezo wa kutoa takribani jigawati 100 ya nguvu za umeme, ikiwa ni ya tatu duniani baada ya China na Urusi. Lakini ni asilimia 9 pekee ya idadi ya raia wa Congo milioni 65 walio na uwezo wa kupata umeme huku katika sekta ya madini inayochangia kiwango kikubwa cha uchumi wa nchi hiyo uhaba wa umeme ukisalia kikwazo kikubwa.

Ramani hii inaonyesha njia ndefu ya kusafirisha umeme kutoka Inga hadi Afrika Kusini
Ramani hii inaonyesha njia ndefu ya kusafirisha umeme kutoka Inga hadi Afrika Kusini

Lakini kwa sasa mpango wa Afrika Kusini kununua umeme kutoka Inga, umefufua mazungumzo ya mradi huo mkubwa. Kwa sasa mashirika matatu makubwa ya kimataifa yanapigania kandarasi ya kujenga bwawa hilo linalojulikana kama Inga ya tatu, na kuuza nguvu ya umeme inayopatikana inayokadiriwa kuwa megawati 4,800.

Hii ni takriban mara tatu ya nguvu ya umeme iliyokuwa inatolewa kwa mabwawa mawili ya Inga, yalioko kwa muda mrefu sasa na yalioharibiwa kutokana na madeni ya serikali ya Congo na wafanyabiashara walioogopa kuwekeza katika miradi hiyo.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Congo, Augustin Matata Ponyo, ametoa taarifa akisema kuwa mradi wa Inga ni mradi unaoweza kuibadilisha Afrika katika karne hii ya 21.

Wakati huo huo kundi moja liitwalo International Rivers limeukosoa mpango huo kwa kutokuwa na manufaa zaidi kwa raia wa nchi hiyo na kutoa wito kwa Benki ya Dunia kufadhili mipango midogo ya kawi kama ya umeme wa kutumia jua ambayo limesema haitadhuru mazingira kwa kiwango kikubwa.

Mwandishi: Amina Abubakar/ Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef