1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bennett angojewa mahakamani

P.Martin (AFPE)16 Februari 2009

Licha ya kukamatwa kwa Roy Bennett.afisa wa ngazi ya juu wa chama cha MDC nchini Zimbabwe,chama hicho huenda kikasita sita kujitoa kutoka serikali ya umoja iliyoundwa kuiongoza nchi na kuikomboa kutoka janga la kiuchumi.

https://p.dw.com/p/Gvb5
** FILE ** In this Monday June 23, 2008 file photo Roy Bennett, a senior member of the Zimbabwean opposition Movement for Democratic Change in neighboring Zimbabwe, speaks during an interview with the Associated Press in Johannesburg, Bennett, an ally of Prime Minister Morgan Tsvangirai who was expected to join Zimbabwe's unity government was arrested Friday Feb. 13, 2009, the party said _ an early indication the country's new political partnership will be rocky. (AP Photo/Denis Farrell, File)
Roy Bennett,afisa wa ngazi ya juu wa MDC aliekamatwa Zimbabwe.Picha: AP

Roy Bennett anayetazamiwa kuapishwa kuwa waziri mdogo wa kilimo juma hili, alikua akitarajiwa kufikishwa mahakamani mjini Mutare leo kujibu mashtaka ya kuhusika na ugaidi na uasi.Wafuasi wa MDC wapatao kama 100 wamekusanyika nje ya mahakama ambako kumetawanya polisi waliobeba silaha nzito.Kesi hiyo imezuka wakati serikali mpya ya umoja wa kitaifa ikianza kufanya kazi leo hii,baada ya kiongozi wa MDC Morgan Tsvangirai kuapishwa waziri mkuu juma lililopita.

Wakati huo huo,Katibu Mkuu wa MDC Tendai Biti alie Waziri mpya wa Fedha wa Zimbabwe alipozungumza na stesheni ya redio ya Afrika Kusini alisema, MDC kitaamua hatua ya kuchukuliwa ikiwa Bennett hatoachiliwa huru.Amesema,waziri mkuu anawasiliana na Mugabe ikitumainiwa kuwa Bennett ataachiliwa huru ifikapo kesho.Chama cha MDC kimetoa mwito wa kumuachilia huru Bennett na wanaharakati wengine wa upinzani waliozuiliwa.

Bennett mwenye miaka 52 alikamatwa siku ya Ijumaa muda mfupi kabla ya mawaziri 35 kuapishwa na Mugabe katika serikali ya umoja.Mawaziri 17 ni kutoka chama cha Mugabe cha ZANU-PF,15 kutoka MDC cha Tsvangirai na 3 ni kutoka tawi dogo la MDC linaloongozwa na Arthur Mutambara alieapishwa kuwa mmoja wa manaibu wawili wa waziri mkuu nchini Zimbabwe.

Roy Bennett ni jina linalochomoza zaidi katika orodha ya baraza la mawaziri la Tsvangirai litakalofanya kazi pamoja na baadhi ya washirika wa kale wa Mugabe. Bennett ni mkulima wa kizungu kutoka eneo la rutuba la Chimanimani karibu na mpaka wa Msumbiji.Yeye alinyanganywa shamba kufuatia mageuzi ya ardhi yaliyofanywa na Rais Mugabe katika mwaka 2003. Mwaka uliofuata Bennett alifungwa jela miezi minane baada ya kumpiga ngumi waziri wa sheria wakati wa mdahalo mkali bungeni uliohusika na mpango wa ardhi. Mwezi uliopita alirejea Zimbabwe baada ya kuishi uhamishoni miaka mitatu kwa hiyari.Alikimbilia Afrika Kusini kuepukana na mashtaka ya kulipia silaha na miripuko ya kuhujumu huduma zilizo muhimu.

Kukamatwa kwa Bennett kunahatarisha uaminifu wa serikali mpya iliyoundwa pamoja na Rais Robert Mugabe kufuatia majadiliano ya miezi kadhaa. Azma ya serikali hiyo mpya ni kuitoa Zimbabwe kutoka janga la kisiasa na kiuchumi.