1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN : Madereva wa treni wagoma tena

18 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Et

Abiria wa treni nchini Ujerumani leo wanakabiliwa na usumbufu mkubwa kwa mara ya pili katika kipindi cha wiki moja wakati madereva wa treni wanapogoma kushinikiza madai yao ya nyongeza ya mshahara.

Kuanzia saa nane usiku chama cha wafanyakazi madereva wa treni nchini Ujerunani GDL wameanza mgomo wao wa huduma za reli za mikoa nchini kote Ujerumani na kuufanya mzozo huo na shirika la reli la taifa nchini Deutsche Bahn ambao umekuwa ukiendelea kwa miezi kadhaa kuzidi kupamba moto.

Shirika hilo la reli la Deutsche Bahn limetowa pendekezo la tano la malipo kwa madereva hao hapo Jumatatu ikiwa ni pamoja na malipo ya mkupuo mmoja wa euro 2,000 na ongezeko la mshahara la asilimia 10 lakini chama cha wafanyakazi madereva kimekataa.

Margaret Suckale mkuu wa idara ya wafanyakazi ya Deutsche Bahn anasema siasa za DGL za viwango vya madai ya mishahara zina madhara kwa wateja,wafanyakazi na shirika.

Chama cha wafanyakazi madereva wa treni GDL kinasema kwamba wanachama wake wanalipwa mishahara midogo kwa kulinganishwa na wenzao katika sehemu nyengine za Ulaya.