1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN: Mkutano kuhusu Mashariki ya Kati washidwa kufikia makubaliano

22 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCPp

Mkutano wa hivi karibuni kuhusu Mashariki ya Kati uliofanyika jana mjini Berlin hapa Ujerumani, ulimalizika bila kufikia makubaliano juu ya hatua inayotakikana ichukuliwe kuhusiana na mpango wa kuundwa kwa serikali mpya ya umoja wa taifa ya mamlaka ya Palestina.

Mkutano huo ulihudhuriwa na pande nne zinazoudhamini mpango wa amani ya Mashariki ya Kati zikiwemo Marekani, Urusi, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya.

Kufuatia mkutano huo wa Berlin, waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, amesema kabla ufanisi wowote kupatikana katika kutafuta amani, sharti Wapalestina wakomeshe machafuko na waitambue haki ya kuwepo taifa la Israel.

Chama tawala cha Hamas katika mamlaka ya Palestina, na chama cha wastani cha Fatah cha rais Mahmoud Abbas, vilikubaliana kuunda serikali ya umoja wa taifa katika juhudi za kuzishawishi nchi za magharibi kumaliza mgomo wao dhidi ya serikali ya Palestina. Waziri mkuu wa Palestina, Ismail Haniyeh, bado yuko katika juhudi za kuunda baraza lake la mawaziri.

Wapalestina wamezitolea mwito dola kuu ziikubali serikali yao ya umoja wa taifa na zianze tena kuwapelekea misaada. Lakini waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, kwa upande wake amesema mgomo dhidi ya serikali ya Palestina unatikiwa uendelee.