1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN : Uamuzi wa kutuma ndege Afghanistan mwakani

23 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCh2

Bado haiko dhahiri iwapo Ujerumani itakubali kuitikia ombi la Umoja wa Kujihami wa Mataifa ya Magharibi NATO kutuma ndege kadhaa za upelelezi aina ya Tornado kusaidia operesheni za kukusanya ushahidi nchini Afghanistan.

Msemaji wa serikali amewaambia waandishi wa habari mjini Berlin kwamba uamuzi juu ya suala hilo haututolewa hadi mwezi ujao.Pia haijulikani iwapo hatua hiyo inahitaji kuidhinishwa na bunge la Ujerumani.Msemaji wa wizara ya ulinzi amesema wanajaribu kuliyakinisha suala hilo.

Mmojawapo wa wabunge wa upinzani wa chama cha Kijani ametishia kupinga jaribio lolote lile la serikali kuridhia ombi hilo bila ya kupigiwa kura na bunge.

Ujerumani hivi sasa ina wanajeshi 2,700 wa Bundeswehr wanaotumika nchini Afghanistan kama sehemu ya Kikosi cha Kimataifa cha Usaidizi wa Usalama ISAF kinachoongozwa na NATO.